Na Adili Mhina, Lindi
Tume
ya Mipango imefanya ziara katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na
uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wilayani
Lindi na kushauri uongozi wa mradi huo kutumia fursa za mikopo ya kilimo
ili kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya mifugo pamoja na kuongeza
uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia kinyesi cha wanyama.
Mradi
huo umekuwa ukizalisha maziwa na nyama kwa ajili ya biashara huku
nishati ya umeme kwa ajili kuendesha shughuli za kiwanda hicho ikiwa
inazalishwa kutokana na kinyesi cha wanayama hao.
Kwa
sasa uzalishaji umepungua baada ya kiwanda kushindwa kuzalisha nishati
ya umeme ya kutosha na kuanza kutegemea umeme wa tanesco ambao kwa
mujibu wa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, Bi Yasinta Mrose
umesababisha gharama za uzalishaji kuongezeka.
Changamoto nyingine ni kuharibika
kwa baadhi mashine zinazotumika kuandaa malisho ya ngo’ombe, ukosefu wa
soko la karibu kwa mazao ya nyama na maziwa, pamoja na uhaba wa maeneo
kwa ajili ya malisho ambapo kwa sasa mradi una zaidi ya ng’ombe 400.
Kutokana
na changamoto hizo, Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence
Mwanri aliueleza uongozi huo kuwa ni vyema wafanye taratibu za kuomba
mkopo hususani katika benki ya kilimo ili waweze kuongeza mtaji,
uzalishaji na kupanua soko.
“Huu
ni mradi mzuri na msirudi nyuma katika uzalishaji wenu, nawashauri mkae
mjadiliane muone namna ya kupata mkopo ili muweze kununua mashine za
kisasa na muongeze uzalishaji. Bila kuchukua hatua hizo mnaweza
mkashangaa mradi unakufa wakati unafaida kwenu na hata kwa wananchi
wanaowazunguka,” alieleza.
Kuhusu
changamoto ya soko la karibu, Mwanri alieleza kuwa uongozi unapaswa
kufikiria kuzalisha maziwa na kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa
na kusafirisha nje ya wilaya ya Lindi kwani soko bado ni kubwa.
Aliongeza
kuwa hatua iliyofikiwa ya kuzalisha umeme wa kutosha kuhudumia shughuli
zote za uzalishaji kiwandani hapo ni nzuri na Serikali inaiunga mkono
jitihada za sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya uchumi ikiwa ni
njia ya kutekeleza malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2016/17-2020/21).
“Nimefarijika
sana kusikia mlikuwa mnazalisha umeme wa kuwatosheleza, mmejitahidi
kutekeleza mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa vitendo. Tume ya Mipango
inatambua na kuunga mkono jitihada zenu hivyo nawasihi shirikianeni na
Halmashauri kufanya kila linalowezekana ili shughuli zenu ziendelee
zaidi ya mlivyokuwa mnazalisha huko nyuma,” aliongeza.
0 comments:
Post a Comment