Na. Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah
Possi ameitaka jamii kuzingatia haki na usawa kwa watu wenye ulemavu nakuondokana na imani potofu za kuona watu wenye ulemavu hawana uwezo wa kufanya shughuli za maendeleo.
Mhe. Possi ameyasema
hayo kwa nyakati tofauti alipotembelea Vituo na Shule zinazohudumia
watu wenye mahitaji maalum vya Nandanga, Rasi Bula, Shule ya msingi
Nyangao mkoani Lindi pamoja na makazi ya wenye ulemavu na Ukoma ya
Mkaseka, Chuo cha wenye Ulemavu cha Mtapika, shule ya Lulindi na Masasi
mkoani Mtwara.
Katika ziara hiyo Mhe.Possi
alisisitiza jamii zibadili mitazamo hasi juu ya masuala ya haki na usawa
kwa watu wenye ulemavu kwa kuwashirikisha katika shughuli zote na
kuwapa vipaumbele vya fursa sawa.
“Ninasisitiza jamii ibadili
mitazamo dhaifu juu ya haki na usawa wa kuwashirikisha watu wenye
ulemavu kwani wana uwezo wa uzalishaji endapo tutawapa fursa sawa kama
ilivyokuwa kwa wakina mama walipoachwa nyuma muda mrefu ila jamii imeona
fursa ndani yao, iwe hivyo hivyo kwa watu wenye ulemavu” alisema.
Aidha Waziri Possi ameweka mkazo juu ya kuwahusisha na kutokuwaona kuwa ni kundi la kuachwa nyuma na kama tegemezi.
“sheria zipo wazi kabisa
zinazotuelekeza juu ya haki na usawa kwa watu wenye ulemavu kwa mujibu
wa matakwa ya Sheria ya watu wenye Ulemavu namba 9 ya mwaka 2010
inayoeleza haki za watu wenye Ulemavu kuwahudumia kwa haki na usawa na
kuboresha maeneo muhimu ikiwemo fursa za kielimu, ajira, kiuchumi na
kijamii,” alieleza.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Joseph Mkirikiti alikiri kuyapokea yote
aliyoeleza Mhe.Waziri katika ziara yake na kuipongeza Serikali kwa
juhudi za kuisaidia jamii bila kujali hali zao na tofauti zao.
“Ninaipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano inayowajali wanyonge na kujali haki zao pamoja na mhe.
Waziri kwa kuona umuhimu wa kututembelea wana Ruangwa na tunaahidi
kukuweka katika kumbukumbu zetu maana umewagusa wakazi wa Mtwara
hususani wazee na watu wenye ulemavu.”Alisisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo.
0 comments:
Post a Comment