Na Godfriend Mbuya
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi amesema maandamano na
mikutano ya hadhara itakayojumuisha viongozi wa kitaifa iliyotangazwa na
CHADEMA haitaruhusiwa kufanyika katika mkao wake tarehe 01.09.2016.
Zambi ameyasema hayo ofisini kwake ikiwa ni siku chache tangu
CHADEMA kutangaza maazimio ya chama chao kwamba wataanza oparesheni ya
kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya kidemokrasia kwa kufanya oparesheni nchi
nzima iliyopewa jina la UKUTA ikiwa na maana Umoja wa Kupinga Udikteta
Tanzania.
''Rais Dkt. John Magufuli ameshatoa agizo la kusitisha
maandamano , hivyo hakuna mtu au kikundi chochote cha siasa ambacho kinaruhusiwa
kufanya maandamano siku hiyo ya tarehe 01.09.2016 na ninamwagiza RPC Mkoa wa
Lindi kuhakikisha hakuna maadamano siku hiyo na watu waendelee na kazi zao kama
kawaida'' Amesema Zambi.
Aidha Zambi amesema mikutano ambayo imezuiwa ni ile ya
viongozi kutoka mikoa mingine na kwenda Lindi , lakini kama ni wabunge wa Lindi
na madiwani wakitaka kufanya mikutano ya hadhara wafanye katika maeneo yao.
''Wabunge wa Lindi na madiwani wanaruhusiwa kufanya mikutano
lakini siyo mtu atoke Arusha au Mbeya kuja kufanya maandamano na mikutano ya
hadhara Lindi'' Amesisitiza Zambi.
0 comments:
Post a Comment