MKUU wa Wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda ameandaa utaratibu wa
kuwakopesha kuku watumishi wote zaidi ya 2,500 wa Halmashauri ya wilaya
hiyo na Manispaa kwa ajili ya kujiongezea kipato na kuboresha afya zao
na ameagiza kila mtumishi kutekeleza hilo.
Utaratibu huo unaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi huu kwa
makubaliano baina ya Mkuu huyo wa Wilaya na wakurugenzi watendaji wa
halmashauri na manispaa ambao mwishoni mwa mwezi huu wataanza na wakuu
wote wa Idara na mapema Julai watachukua watumishi wengine.
Akizungumza na gazeti hili juzi, alisema wameanzisha mradi wa kuku
wilayani humo kwa ajili ya kuviwezesha vikundi, wanawake, vijana na
watumishi wa serikali kujiongezea kipato na wamekubaliana kila mkuu wa
idara achukue kuku wasiopungua 30 mwisho wa mwezi huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lindi, Jomaary
Satura, halmashauri hiyo ina watumishi 1,741. Mkuu wa Wilaya alisema kwa
upande wa Manispaa kuna watumishi 950 na watapaswa kuchukua kuku na
kurejesha fedha kwa awamu kwa kipindi cha miezi sita.
“Hii ni amri halali, si hiari, hatutaki kuona mtumishi akilalamika
hali ngumu ya maisha, hii falsafa ya mkuu wa nchi, Rais John Magufuli ya
Hapa Kazi Tu ni kwa wote, hivyo nimeamua kuwakopesha kuku watumishi
wote wa Lindi,” alisisitiza Nawanda.
Akifafanua zaidi, alisema wana mradi wa kuku zaidi ya 50,000 na
watumishi wa Lindi watachukua kuku pamoja na viuatilifu zikiwamo dawa na
atakuwa na hiari ama ya kuwala kuku wote ama kufuga na baadaye kuuza
mayai na mengine kula kuimarisha afya zao.
“Kwa mfano, kuku mmoja anauzwa kwa shilingi elfu tatu, akichukua kuku
30 ni shilingi elfu tisini, akilipa kwa miezi sita kila mwezi itakuwa
ni shilingi 15,000. Akiamua kula wote sawa, akifunga kwa tija apate
mayai, vifaranga na kuuza pia sawa,” alisema.
Alipoulizwa haoni kama ni kumlazimisha mtu kufanya jambo asilolitaka
ikiwa itakuwa amri kwa wote, alisema ndio maana wameweka uhuru kwa
mhusika akitaka kuchinja kuku wote ni sawa ilimradi asije kusema
hakuwezeshwa.
Alisema anataka wakuu hao wa idara na watumishi kuwa mfano katika
mradi wa ufugaji kuku ili kusaidia kuielimisha jamii inayowazunguka
faida na umuhimu wa ufugaji huo kwa uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa
ujumla.
Mmoja wa wakuu wa idara katika halmashauri hiyo, Mkuu wa Idara ya
Mipango Miji na Maliasili, Michael Mlyambongo, alisema yeye atachukua
kuku 100 na matarajio yake ni kufikisha kuku 500 ili kujiongezea kipato.
Meneja wa Mradi wa Kuku, Salma Zahoro alisema wanajitahidi kuinua
vipato vya Watanzania.
Chanzo Gazei la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment