Na
Anna Nkinda – Maelezo, Masasi
Wanafunzi wa kike wilayani Masasi wametakiwa kuachana na tamaa za maisha
zinazowapelekea kujiingiza katika mapenzi kabla ya wakati na hivyo kupata
ujauzito unaowasababisha kukatiza masomo yao.
Ushauri
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
wananchi wakiwemo wanafunzi waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya gari
la wagonjwa la Hospitali ya Mkomaindo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya
Mkuu wa wilaya hiyo.
Mama
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema
kuna baadhi ya wanafunzi wanapenda maisha mazuri wakati wazazi wao hawana uwezo
na hivyo kujiingiza katika mapenzi ili wapate fedha zitakazowafanya wanunue
vitu wanavyohitaji.
“Wengine
mnadiriki kufanya mapenzi na watu wazima waliowazidi umri msifanye haya
mambo kabla ya wakati. Ridhikeni na maisha ya wazazi wenu matokeo yake mtapata
mimba na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
“Nawasihi
wanangu msiruhusu mazingira ya kupata mimba mkiwa shuleni bali someni kwa
bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu kwa kufanya hivyo mtakuwa na
maisha mazuri hapo baadaye. Wavulana walindeni dada zenu ili
wasidanganywe na wanaume, nanyi pia someni muache tabia ya utoro hii itasaidia
kuwa na Masasi ya wasomi”, alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa
mujibu wa Taarifa ya Maendeleo ya Wilaya ya Masasi bado kuna tatizo kubwa
la wanafunzi wa kike kuacha shule kutokana na ujauzito. Mwaka 2013
wanafunzi 35 walipata ujauzito na mwaka 2014 waliopata ujauzito ni 22 na
hivyo kukatiza masomo yao.
Akisoma
taarifa hiyo Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu ambaye ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya
Masasi Sauda Mtondoo alisema kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ujauzito
ni kutokana na kuanzishwa kwa vilabu vya wapinga mimba mashuleni na watuhumiwa
wote wa tukio hilo kufikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.
“Changamoto
tunazokutana nazo ni walezi kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria pindi
watoto wao wanapopata ujauzito, kesi nyingi zinamalizwa kinyemela, watuhumiwa
kutoweka pindi wanapohusishwa na ujauzito wa mwanafunzi husika”, alisema
Mtondoo.
Mkuu
wa wilaya huyo aliitaja mikakati waliyonayo ni kutoa elimu kwa watoto ili
wazielewe stadi za maisha, kuimarisha kitengo cha ushauri na unasihi katika
shule za sekondari kwa kuwa na walimu na malezi na kuanzishwa kwa klabu za
wasichana katika shule zote za Sekondari kwa mantiki ya kupunguza utoro na
mimba za utotoni.
Wilaya
hiyo ina jumla ya shule za sekondari 37 kati ya hizo za Serikali ni 35 na
binafsi mbili na shule za msingi 159 zenye wanafunzi 68,316.
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment