Mke wa Rais
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mama Salma Kikwete
akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Jamhuri lililoko katika
Kata ya Jamhuri, Lindi Mjini kwenye mkutano wa ndani tarehe 17.3.2015.
PICHA NA JOHN
LUKUWI.
Na
Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wanafunzi wametakiwa kujiepusha na vitendo vitakavyowapelekea kupata
maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni jambo
litakalowafanya wakatize masomo na hivyo kutotimiza ndoto za maisha yao.
Rai
hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Mkonge iliyopo wilayani humo.
Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuna baadhi ya
wanafunzi wanajiingiza katika mapenzi kabla ya wakati kwa kufanya hivyo
wanakumbana na mimba za utotoni na ugonjwa wa Ukimwi.
“Mimba
na Ugonjwa wa Ukimwi vinapatikana kwa njia ya kufanya mapenzi
yasiyo salama, msikubali kudanganywa na watu wazima ili muwe wapenzi wao
watawaharibia maisha yenu.
“Sote
tunajuwa kipindi cha balehe kinasumbua kijana anatamani kufanya
kila kitu kilichopo mbele yake, epukeni majaribu haya! Mkiwa
shuleni msifanye mapenzi wakati wake bado haujafika, msichana na mvulana
mshirikiane katika masomo tu na siyo kufanya mapenzi”, alisema Mama Kikwete.
MNEC
huyo aliwahimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika
masomo yao kwa kufanya hivyo wataweza kuepukana na ujinga, maradhi na umaskini.
Alisema,
“Ili muweze kuwa na maendeleo ya elimu ni lazima muache utoro, msome kwa
bidii, msome katika makundi ya watu wenye uelewa wa masomo tofauti wasiozidi
saba pia nidhamu iwe msingi wa maisha yenu kwa kufanya hivyo mtafaulu.
“Wazazi
wenu wamewasaidia kwa kuwapeleka shule , ukiwa na jitihada za makusudi
utafanikiwa wekeni malengo katika maisha yenu, tengenezeni ratiba
ya kujisomea nyumbani na walimu wenu wakiwapa mazoezi ya masomo mkafanye
nyumbani mjitahidi kumaliza kwa wakati”.
Kwa
upande wake Kaimu Mkuu wa wilaya ya Lindi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kilwa
Abdallah Ulega aliwaambia wanafunzi hao kuwa wao ni viongozi lakini hadi wafike
huko kuna milima na mabonde wanayotakiwa kuyavuka.
“Fanyeni
jitihada katika masomo yenu kwani hakuna mtu aliyezaliwa na akili nyingi
kuliko mwingine , ukiwa na akili ni jitihada zako binafsi, elimu ni vita
lazima uishinde na hakuna mchawi katika masomo. Mkifanikiwa katika hili mtakuwa
viongozi wazuri hapo baadaye”, alisema Ulega.
Naye
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa aliwasihi vijana hao kusoma kwa
bidii ili waweze kuzitumia rasilimali zilizopo mkoani humo ikiwa ni pamoja na
kufanya kazi za kitaalam katika sekta gesi kwani wasiposoma kazi hizo zitafanywa
na watu wengine na wao watabaki kulalamika.
Akisoma
taarifa ya shule , mkuu wa shule mwalimu Bahia Abubakar alisema
shule hiyo yenye wanafunzi 643 wa kidato cha kwanza hadi cha nne na walimu 39
ilianzishwa mwaka 1966 ikiwa ni shule binafsi inayomilikiwa na watu wenye asili
ya Asia lakini mwaka 1995 ilikabidhiwa kwa Serikali.
Alizitaja
changamoto zinazowakabili ni upungufu wa walimu sita wa masomo ya sayansi na
hisabati, uchakavu na upungufu wa majengo, utoro wa rejareja kwa wanafunzi,
ukosefu wa uzio, upungufu wa samani na nyumba za walimu, wazazi kutoshiriki
kikamilifu katika malezi na kuwahamasisha watoto kupenda shule.
Mwalimu
Bahia alisema, “Mafanikio tuliyoyapata ni maendeleo ya taaluma yanaendelea
kupanda mwaka hadi mwaka kwani matokeo ya kidato cha pili yamepanda kutoka
asilimia 30.5 kwa mwaka 2011 hadi 90 kwa mwaka 2014 na matokeo ya kidato cha
nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 35 kwa mwaka 2011 hadi 68 kwa mwaka
2014.
“Tumefanikiwa
kuhamasisha wazazi kuchangia fedha kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi uji shuleni
na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa utoro wa rejareja pia juhudi zinaendelea
ili kuwapatia chakula cha mchana, tunaendelea kutoa motisha kwa walimu ambao
masomo yao yamefanya vizuri katika mitihani ya taifa na hatuna upungufu wa
walimu wa masomo ya sanaa”.
Mama
Kikwete aliwapa wanafunzi hao zawadi ya vifaa vya bendi ya shule, kutokana na
tatizo la maji shuleni hapo aliahidi kuchimba kisima, aliahidi kuwapa wanafunzi
mipira na jezi na kuwachangilia shilingi 1,670,000/= kwa ajili ya ziara ya
masomo wilayani Bagamoyo.
Pia
alikamilisha ahadi yake aliyoiahidi mwezi uliopita kwa shule ya Sekondari ya
Angaza na kuwakabidhi wanafunzi pamoja na walimu vifaa vya bendi ya shule
na mabati 100 ambayo yatatumika kuezeka chumba kimoja cha maabara kati ya
maabara tatu zinazojengwa.
Wakati
huo huo MNEC Mama Kikwete alitembelea tawi la Jamhuri na
kuwataka viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi hilo kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia
kura katiba inayopendekezwa na kuwachagua viongozi wakati wa uchaguzi
mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
“Katika
wilaya yetu kila kata imepewa nakala za katiba inayopendekezwa 300 , tumieni
muda wenu kuzisoma na kuelewa mambo yaliyoandikwa, wakati ukifika mkaipigie
kura ya ndiyo kwani ni katiba bora kwakuwa imegusa maisha ya kila mtanzania”,
alisisitiza Mama Kikwete.
Aidha
aliwahimiza wajumbe hao kwenda Hospitali kupima saratani za tezi dume na shingo
ya kizazi ili kama watakutwa na dalili za ugonjwa katika hatua za awali
watatibiwa na kupona kabisa.
Mama
Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni
pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya mwaka 2010 . Hadi sasa ameshatembelea matawi yote 82
yaliyopo wilayani ya Lindi mjini.
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment