Home » » MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE WASISAHAU JUKUMU LAO LA MALEZI YA FAMILIA‏

MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE WASISAHAU JUKUMU LAO LA MALEZI YA FAMILIA‏


Na Anna Nkinda –  Maelezo, Lindi
 Wanawake kama wazazi wametakiwa kutimiza jukumu lao la  malezi ya  familia kwani  wengi wao kutokana na hali halisi ya maisha wameacha kufanya kazi hiyo na kuwaachia wadada wa kazi.

Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho  katika matawi ya Barabara ya Mchinga, Mitandi Magharibi na Kusini na Rutamba.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kutokana na hali halisi ya maisha baadhi ya wamama wanamajukumu mengi ya kazi na jukumu la malezi ya watoto wamewaachia wa dada wa kazi jambo ambalo siyo zuri kwa makuzi ya mtoto.

“Tunajua kutokana na hali halisi ya maisha wanawake wengi wanahangaika kufanya kazi ili wapate fedha zitakazosaidia kuinua kipato cha familia lakini hata kama unamajukumu mengi  jioni ikifika jitahidi ukae na familia yako  mle  pamoja chakula cha jioni  kwa kufanya hivyo utajua matatizo yanayowakabili.

Imefikia hatua mama akimlisha chakula mtoto wake aliyemzaa yeye mwenyewe anakataa kula lakini akilishwa na dada wa kazi anakula na wamama wengine hata chai ya kunywa mmewe anatengewa na dada wa kazi badilikeni jamani”, alisisitiza Mama Kikwete.

MNEC huyo pia aliwasisitiza viongozi hao kupendana, kusaidiana na kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa kufanya hivyo watakuwa na maendeleo katika maisha yao na kuvisaidia  vizazi vyao.

Akiwa katika tawi la Angaza mlezi huyo wa CCM wilaya ya Lindi mjini pia aliwahimiza viongozi hao kutoogopa kupima saratani za tezi dume na shingo ya kizazi  kwani  magonjwa hayo yakigundulika katika hatua ya awali yanatibika , mgonjwa anapona na kurudi katika hali yake ya kawaida.

Mama Kikwete alisema, “Kuna saratani ya tezi dume hii inawapata wanaume kuanzia umri wa miaka 45 na kuendelea. Kwa wanawake kuna saratani  ya shingo ya kizazi,  nawaomba msifanye masihara katika hili nendeni Hospitali mkapime kwani ukijua tatizo madaktari   watatengeneza mazingira ya kutibiwa na  kuliondoa tatizo hilo”.

Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010. Hadi sasa ameshatembelea matawi 78 kati ya  82 yaliyopo wilaya ya Lindi mjini.

    


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa