Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
13/2/2015 Wanafunzi wa kike nchini
wameaswa kutoogopa kusoma masomo ya sayansi kwani masomo hayo siyo magumu
ukilinganisha na mengine wanachotakiwa kufanya ni kuzishika na kuzijua
kanuni za somo husika.
Rai hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya
Sekondari ya Angaza iliyopo wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema mwanafunzi anayesoma masomo ya sayansi
akizishika kanuni anafanya vizuri katika masomo yake tofauti na mwanafunzi wa
masomo ya sanaa na kutoa mfano kama mwanafunzi anataka kujua hesabu ni lazima
kila siku kabla hajalala afanye mazoezi kwa maswali yasiyopungua 10.
Kwa upande wa uongozi aliwataka
wasichana kutoogopa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi kwani wakianza
uongozi katika umri mdogo watakuwa viongozi wzuri hapo baadaye.
MNEC huyo aliendelea kuwaasa
wanafunzi hao na kuwaambia kuwa wao ni ndugu na wakiona mwenzao mvulana
au msichana amesimama na mtu wa jinsia tofauti katika mazingira tatanishi
wamkanye aache tabia hiyo kwani kilichowapeleka shule ni
kusoma na siyo kufanya mapenzi.
“Elimu ni nguzo ya maisha ni lazima
mjitambue nyie ni kina nani, mnafanya nini na mnataka kuwa nani
hapo baadaye. Someni kwa bidii, waheshimuni na kuwasikiliza walimu wenu kwa
kufanya hivyo mtafaulu na kufika chuo kikuu.
“Mkiwa wasomi wazuri mtawezaa
kuzitumia fursa zilizopo katika mkoa wetu ikiwa ni pamoja na kuajiriwa katika
sekta mbalimbali ikiwemo ya gesi”, alisisitiza Mama Kikwete.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi
Mzee Alli Mtopa alisema Dunia ya leo ni ya wasomi hivyo basi ni lazima
wanafunzi hao wasome ili wafanye kazi katika sekta ya gesi inayopatikana mkoani
humo kwani wasiposoma kazi za kitaalamu zitafanywa na watu wengine
na wao watabaki kufanya kazi za vibarua na mwisho wake wataandamana
kuzuia gesi isitoke.
Akisoma taarifa ya shule hiyo
mchanganyiko Mkuu wa shule mwalimu Upendo Muro alisema shule hiyo ambayo ni ya
kata ilianza mwaka 2008 ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne 359 na
walimu 25.
Mwalimu Muro alisema kwa upande wa
wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga katika shule shule
hiyo kwa mwaka huu ni 102 walioripoti ni 87 kati yao wanawake ni 45 na
wanaume ni 42.
“Changamoto zinazoikabili shule yetu
ni upungufu wa majengo, nyumba za walimu, vifaa vya maabara na
walimu wa masomo ya sayansi ambayo ni kemia, fizikia na hesabu, ukosefu
wa umeme, maji, kutokuwa na jengo la maabara, na ukosefu wa vyoo vya
walimu”, alisema Mwalimu Muro.
Aliyataja mafanikio waliyoyapata
kuwa ni pamoja na kuwarudisha shuleni wanafunzi watoro, matokeo ya kidato cha
pili na cha nne yanazidi kuwa mazuri kadri miaka inavyokwenda,
wanafunzi wanakunywa uji na mchakato unaendelea ili wale chakula cha mchana.
Wanafunzi wa kidato cha nne
waliohitimu mwaka jana wote walifanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa
vitendo na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana shule imeweza
kutoa wanafunzi waliojiunga na kidato cha tano katika masomo ya PCB
wawili, PCM mmoja na HGL wawili.
Akiwa shuleni hapo alikagua ujenzi
wa vyumba vitatu vya maabara za fizikia, kemia na bailojia na kuahidi kuchangia
mabati 100 pia aliahidi kuwaletea wanafunzi vifaa vya bendi ya shule.
Aidha Mama Kikwete alifanya vikao na
viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi ya
Angola, Majani Mapana na Angaza yaliyopo kata ya Wailesi na kuwahimiza
wazazi wawasisitize watoto waone umuhimu wa kuwa na elimu.
“Kina mama zungumzeni na watoto wenu
wa kike ili wasijihusishe na mapenzi wawapo shuleni kwani mimba ni sumu,
mtoto akipata ujauzito atakatisha masomo yake na kutotimiza ndoto zake. Nanyi
kinababa msipokee mahari za watoto wenu ambao ni wanafunzi subirini
hadi watakapomaliza masomo yao”, alisisitiza.
Kuhusu ufanyaji wa kazi za nyumbani
aliwaambia viongozi hao ni muhimu watoto wote wa kike na wa kiume wakafundishwa
kazi hizo na siyo kazi hizo zikafanywa na mtoto wa kike peke yake jambo
litakalomfanya kukosa muda wa kujisomea pindi arudipo shuleni.
Katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Kata ya Wailesi Mama Kikwete aliwaambia wananchi kwamba Serikali ya
CCM imeboresha elimu kwa kujenga shule za Sekondari za Kata ambazo hivi sasa
hata watoto kutoka familia maskini wanapata elimu ya Sekondari tofati na
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Mama Kikwete alisema, “Hivi sasa
hakuna mtoto anayefaulu na kukosa shule, zamani katika mkoa huu kulikuwa
na Sekondari mbili tu ya Lindi Sekondari kwa wanafunzi waliofaulu darasa la
saba na Mkonge kwa wanafunzi waliofeli, na kujiunga na shule hii ilikuwa
ni lazima mzazi awe na fedha ya kulipa.
“Mtoto akifeli usihangaike
kumtafutia shule ya kulipia bali mpeleke elimu ya ufundi kwani siyo wote
watakaosoma elimu ya sekondari wengine watasoma masomo ya ufundi ambayo yatawasaidia
kuweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe”.
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa
ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na
viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 .
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment