Home » » MILIONI 721/- KULIPA FIDIA WANANCHI WA LINDI

MILIONI 721/- KULIPA FIDIA WANANCHI WA LINDI

SERIKALI kupitia Wizara yake ya Maji imeipatia Mamlaka ya Maji Manispaa ya Lindi (LUWASA) sh.721,241,000 zitakazotumika kulipa fidia kwa wananchi watakaochukuliwa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi mpya wa maji, kutoka maeneo ya Ngíapa kwenda mjini Lindi.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Nassoro Hamidi, alipokuwa akielezea mikakati ya kuboresha huduma mbalimbali kwa jamii inayoendelea kutekelezwa na Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara ya Katibu mkuu, Abdulrahmani Kinana.

Akiwasilisha maelezo yake hayo, Dkt. Hamidi alisema fedha hizo zitatumika kulipia fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa matangi ya kuhifadhia maji na upitishaji wa mabomba.

Dkt. Hamidi amesema kwa sasa mahitaji ya huduma ya maji katika mji wa Lindi ni lita milioni 500, lakini yanayopatikana kwa hivi sasa ndani ya mji huo ni lita milioni 250.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Lindi, alisema upungufu huo unachangiwa zaidi na kupungua kwa maji katika vyanzo vyake mbalimbali vikiwemo vya Kitunda, Mmongo na Liwayawaya.

"Kuibuliwa kwa chanzo hiki kipya cha Ngíapa, kulitokana na kupungua maji kwa vyanzo vya awali ndipo utaratibu ulipofanywa kutafuta chanzo kingine cha Ngíapa," alisema Dkt. Hamidi.

Dkt.Hamidi alisema mradi huo utakapokamilika mwaka ujao wa 2015, utasaidia kuongeza idadi ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wakazi wa mji huo wa Lindi, kutoka lita milioni 250 za sasa hadi lita 750 milioni.

Akizungumza na wakazi wa mji huo, Katibu mkuu Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahmani Kinana, amewataka wananchi kulinda miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa maji ili iweze kuwasaidia kuondokana na kutumia maji yasiyo salama kwa binadamu.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa