Home » » MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIGA KURA KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA‏

MAMA SALMA KIKWETE AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUPIGA KURA KATIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA‏

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika  uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za Uenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa katika kata za Ndoro na Mikumbi zilizopo wilaya ya Lindi mjini.

Alisema kuna baadhi ya watu hawajiandikishi na wengine siku ya uchaguzi ikifika hawaendi kupiga kura, wanabaki kulalamika viongozi hawafai. Lakini kama wangeshiriki katika uchaguzi kusingekuwa  na malalamiko kwa kuwa wangekuwa  wamechagua viongozi wanaowataka.

 “Siku ya uchaguzi ikifika amkeni mapema mkapige kura na msipoteze kura zenu kwa kuchagua watu wengine, chagueni viongozi wa   CCM ambao chama chetu kimefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, ujenzi wa shule na kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu”, alisema Mama Kikwete.

Aidha MNEC huyo pia aliwasisitiza wanachama hao wakati wa kujiandikisha majina katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali Kuu ukifika  wawahamasishe wananchi  wakajiandikishe ili waweze kuwachagua viongozi wao.

Akiwa katika  mkutano wa kampeni uliofanyika  mtaa wa Mto Mkavu Mama Kikwete aliwanadi  kwa wananchi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa kutoka Kata ya Mbanja.

Aliwasihi vijana kubadilika na kujifunza historia ya nchi yao hapo ndipo watajua wapi nchi imetoka na wapi inakwenda kwani hivi sasa kuna watu wanapita na kuwadanganya hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana ukilingamisha na miaka ya nyuma.

Mama Kikwete alisisitiza, “Lazima mtambue kuwa Serikali ya CCM imeleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kujenga barabara na hivi sasa kutoka  Lindi hadi Dar es Salaam kwa gari dogo unatumia  masaa matano na unaweza kwenda na kurudi, kwa basi siyo zaidi ya masaa saba. Leo watu wanapita na kuwadanganya hakuna maendeleo yaliyofanyika jambo ambalo siyo kweli”.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii alisema kuna propaganda zinazosambazwa na wapinzani kuwa Serikali imesogeza mbele  siku  ya uchaguzi hadi tarehe 17 kitu ambacho  siyo sahihi kwani uchaguzi utafanyika tarehe 14 mwezi huu kama ilivyopangwa.

Muksini alimalizia kwa kuwaomba wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa viongozi kwani kuna watu wanapita na kuwadanganya wasiwachague wagombea  wenye dini na  makabila tofauti na yao wasiwasikilize, Tanzania haina dini wala kabila watu wote ni sawa na kuwasisitiza kuwachagua viongozi wa CCM ambao watawaletea maendeleo.

Katika mkutano huo wa kampeni  wanachama wanne kutoka chama cha Wananchi (CUF) walimkabidhi Mama Kikwete kadi za chama hicho na kujiunga na  Chama Cha Mapinduzi.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa