Home » » MIKUTANO YA KISIASA LINDI, MTWARA RUKSA

MIKUTANO YA KISIASA LINDI, MTWARA RUKSA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeondoa zuio la mikutano ya vyama vya siasa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Mathias Chikawe, awali Serikali ilipiga marufuku mikutano hiyo Mei 2012.

Alisema zuio hilo lilitokana na vurugu za wananchi waliokuwa wakipinga ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam hali ambayo ilisababisha kuvunjika kwa amani na utulivu katika mikoa hiyo.

Aliongeza kuwa, katika vurugu hizo watu kadhaa walifariki dunia na wengine kujeruhiwa ambapo magari na nyumba, vilichomwa moto.

"Serikali imeamua kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa katika mikoa hii baada ya kuridhika kuwa hali ya amani, utulivu imerejea; hivyo mikutano hiyo inaweza kuendelea kwa wahusika kufuata sheria na utaratibu uliowekwa.

"Jeshi la Polisi nchini litaendelea kutoa ushirikiano katika uendeshaji wa mikutano ya kisiasa inayoendelea katika mikoa yote nchini ambapo vibali vitatolewa kutokana na mazingira ambayo yatakuwepo kwenye eneo husika ambalo chama kimeomba kibali," alisema.

Bw. Chikawe alisema Serikali inaamini vyama vya siasa vitatumia fursa hiyo kuendesha mikutano yao kwa amani na utulivu wakishirikiana na jeshi hilo kama taratibu za uendeshaji mikutano zinavyoelekeza

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa