Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kundi la vijana wasiofahamika kutoka mjini Liwale, mkoani
Lindi, wamevamia Kituo cha Polisi Lionja na kuwazidi nguvu askari, kabla
ya kumtorosha mtuhumiwa wa mauaji na kisha kumuua na mwili wake
kuuchoma moto.
Aliyeuawa ametambulika kwa jina la Issa Mfaume
(31), mkazi wa Likongowele aliyekuwa akishikiliwa kituoni hapo kwa
tuhuma za mauaji ya Zalali Lunje (27) kwa kumchoma kisu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Rainata Mzinga
alisema tukio hilo lilitokea jana saa nne asubuhi, karibu na Kituo cha
Mabasi cha Liwale.
Baadhi ya mashuhuda bila kutaka kutaja majina yao,
waliliambia gazeti hili kuwa, vijana hao wakiwa na pikipiki walikwenda
kituoni hapo na kuwatisha polisi kabla ya kumtorosha mtuhumiwa huyo wa
mauaji.
Baada ya kufanikiwa kumtorosha mtuhumiwa
aliyedaiwa kufanya mauaji mwishoni mwa wiki iliyopita, walimpeleka hadi
eneo analotuhumiwa kufanya mauaji na kisha kuanza kumpa kichapo.
“Niliona kundi la vijana wakimpiga sehemu
mbalimbali mwilini, aliishiwa nguvu na baadaye walimchoma moto hadi
mwili wake kuteketea kabisa,” alisema shuhuda ambaye hakutaka jina lake
kuandikwa gazetini.
Kamanda Mzinga alisema jeshi lake linawasaka
wahusika wa mauaji na kisha kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma za
kujichukulia sheria mkononi.
Amewataka wananchi kuepuka utamaduni wa
kujichukulia sheria mikononi. “Sheria zipo, lazima zifuatwe na
watakaokwenda kinyume wanatafuta matatizo,” alionya Mzinga.
Chaonzo:Mwananchi
Chaonzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment