Home » » UWT wakemea, walaani ushoga

UWT wakemea, walaani ushoga

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani hapa umekemea vikali vitendo vya ushoga vilivyokithiri jijini huku wanawake wakidaiwa kuwa ndio vinara wa kutoa mialiko kwa mashoga katika sherehe mbalimbali.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Janeth Masaburi aliwalaumu wanawake wanaoalika mashoga kwenye sherehe na kusema jambo hilo ni la aibu kwa taifa.
“Wanawake wenzetu mnatutia aibu. Mnaalika mashoga ili waionyeshe nini jamii?” alihoji wakati akihutubia wanawake wa Kata ya Vingunguti wilayani Ilala.
Alisema: “Kwenye sherehe unakutana na wanaume wamevaa magauni aina ya madila wanacheza kama vile wanawake, lakini ukiuliza unaambiwa wamealikwa kwenda kutumbuiza huku wanawake wakiongoza kutoa mialiko hiyo.”
Masaburi alisema UWT hauwezi kukaa kimya ikishuhudia matukio hayo ya aibu bali, itaendelea kukemea vitendo hivyo vinavyoharibu malezi ya watoto.
“Kwenye sherehe hizo unakuta kuna watoto na hivyo wanashuhudia vitendo hivyo vichafu vikifanyika. UWT tunalaani kwa nguvu zote vitendo hivyo,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, Masaburi alitoa wito kwa wanawake kugombea nafasi za juu za uongozi utakaofanyika Septemba mwaka huu.
Alisema wanawake wenye uwezo ‘wapambane’ ili kuhakikisha kwamba wanachukua nafasi za juu katika serikali za mitaa.
“Wanawake ni viongozi makini na mnaweza kufikia malengo yenu ikiwa mtafanya uamuzi wa kugombea nafasi za uongozi,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Asah Simba aliwataka wafuasi wa chama hicho kujiandaa na chaguzi hizo ili waweze kupata ushindi wa kishindo.
Alisema wakati kikundi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakipita ‘kupiga’ propaganda za Katiba wanaCCM wajiandae kwa uchaguzi huo ili waweze kushinda mitaa yote
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa