Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tumekuwa tukiandika kwa muda mrefu sana kuhimiza utalii wa ndani
na wageni kutoka nje. Pia kuhusu umuhimu wa kuzilinda rasilimali na
amali zetu za kiutamaduni na kihistoria na kimazingira (wanyama na
misitu). Kwa ufupi nitaeleza utalii unaweza kuwa na faida gani kwa jamii
na taifa.
Utunzaji wa mazingira na uoto kwa ajili ya utalii
licha ya kuliingizia Taifa fedha za ndani na za kigeni kwa kutokana na
wageni watembeleao vivutio. Lakini utunzaji huo husaidia pia kuleta mvua
na kutunza maji ambavyo ni muhimu kwa wakulima na wafugaji. Kwa hiyo
utalii huweza kuwa na faida kwa njia ya namna hiyo ya mzunguko kwa
wananchi na kukuza hali ya kipato chao katika shughuli zisizo za
kitalii.
Ni muhimu sana kwa Serikali kujenga miundombinu
inayosaidia kukuza utalii, lakini wananchi wanaweza kuwa na jukumu kubwa
zaidi la kuimarisha miundombinu kama usafiri, nyumba za kulala wageni
au sehemu za burudani (kambi za utalii, mikahawa na vyakula vya kiasili)
kwa ajili ya kuwavutia watalii. Tanzania imebarikiwa sana na vivutio
vya utalii ambavyo havitumiwi, kama wananchi wangejishirikisha vizuri
ingekuwa rahisi kwa nchi kuvitunza na kuviuza vivutio vya utalii. Mto
Pangani, kwa mfano, unaweza kutumika vizuri sana kwa ajili ya Utalii wa
kihistoria na wa kimazingira. Wananchi wanaweza kuhamasishwa kuwekeza
katika miundombinu hasa usafiri na maeneo ya kujihifadhi na
kuwasafirisha watalii kwenye mto kuona mazingira na maeneo ya
kihistoria. Maeneo ambayo wananchi wameshirikishwa vizuri faida ya
utalii kwa jamii huonekana wazi, ili mradi ushirikishwaji huo usiwe wa
kudhalilisha mila na desturi zetu. Lakini hapa tunaona utalii ukiongeza
ajira binafsi kwa wakazi. Unguja mjini inatoa mfano mzuri kwa hivi
karibuni vijana kuanzisha miradi ya usafirishaji wa watalii kwenda
kwenye visiwa vyenye vivutio vya utalii vilivyo jirani.
Watalii huja eneo fulani kutafuta vitu ambavyo
kwao hawana, au kula vyakula ambayo kwao havipo, na kuburudika kwa
ujumla. Kwa kuweza kupata hayo wanayotafuta kutoka maeneo ya utalii,
nchi wapokeaji watalii hulazimika kukuza ubora wa vyakula, au ubora wa
maeneo ya kulala ili kuweza kufikia viwango vya kimataifa.
Kwa njia hiyo utalii hukuza uchumi na kukuza tabia
za usafi, kuhimiza ujenzi wa kisasa wa majengo, au kuwa na huduma za
kisasa katika maeno fulani fulani ili kuwavutia watalii na hivyo
kuongeza ajira. Tumesema kuwa kama nchi inajipanga vizuri katika utalii
kuna uwezekano wa kukuza aina fulani ya vyakula, hasa matunda na
mbogamboga ambavyo watalii huvipenda sana.
Matunda kama tufa, machungwa na ndizi, na mengine
yasiyo na asili ya Ulaya hupata soko sana maeneo ya utalii. Kwa hili
serikali hulazimika kuweka sera nzuri za kilimo na kuhamasisha ulimaji
mazao ambayo yanayoweza kuongeza pato la wananchi kupitia watalii.
Kwa sasa hivi mifumo ya utangazaji ndani na nje ya nchi haina uchagamano unaoweza kuleta tija.
Ni bora kama watalii wanapokuwa wanatembelea nchi
wakajua kuwa pamoja na kuona utalii wa wanyama, kwa mfano, bado kuna
maeneo ya historia yaliyo jirani. Pia wananchi wana utamaduni wao ambao
wangeweza kuwaonyesha au kuwauzia wageni.
Kwa vile wananchi wengi walio katika maeneo ya
utalii hawajahamasishwa hawaelewi namna gani wanavyoweza kujiingiza
katika shughuli ambazo wangewauzia watalii.
Bagamoyo kwa mfano, wangeweza kuhamishwa kujiunga
katika shughuli za upikaji chakula, au uchezaji na kurekodi ngoma za
asili kwa ajili ya watalii. Wananchi wamebaki nao wakiwa waangaliaji
watalii wanaotembelea maeneo yao bila kupata faida ya moja kwa moja
kupitia shughuli ambazo wangezifanya.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment