Pan African Energy Tanzania (PAT)
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE, umebaini kuwa, kijiji hicho kilichopo katika Kisiwa cha Songosongo, umbali wa takriban maili 16 kutoka bandari ya Kilwa Kivinje, kimeambulia Sh. milioni 86 tu kati ya Sh. milioni 309 walizotakiwa kulipwa katika kipindi cha kuanzia Aprili, 2012 hadi Desemba 2013.
Kwa mujibu wa sheria ndogondogo za Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuhusiana na ‘service levy’, iliyopitishwa mwaka 2010, Songosongo hutakiwa kupata asilimia 20 ya kodi hiyo ya huduma inayolipwa kila baada ya miezi mitatu na wawekezaji wa gesi Songosongo, Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT).
Taarifa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (DED) inaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana, jumla ya Sh. bilioni 1.749 zilishalipwa na PAT; huku Sh. milioni 200 kati ya hizo zikielezewa kuwa ziko mikononi mwa manispaa moja nchini ambako wanaendelea kuzifuatilia.
Inadaiwa kuwa awali, jumla ya Sh. milioni 600 za service levy ya gesi ya Kilwa zililipwa kimakosa katika manispaa hiyo isiyokuwa ya mkoa wa Lindi na baada ya kuziulizia, Kilwa walilipwa Sh. milioni 400 tu.
Taarifa ya mapato ya ‘service levy’ ya gesi wilayani Kilwa inaonyesha kuwa ilianza kulipwa kwao Aprili 14, 2012 na hadi kufikia Desemba, 2013, tayari halmashauri ya wilaya hiyo ilishapokea Sh. bilioni 1.549.
Ukokotoaji wa asilimia 20 ya fedha hizo unaonyesha kuwa kiasi kilichotarajiwa kulipwa kwa kijiji cha Songosongo ni zaidi ya Sh. milioni 309, ingawa hadi sasa wameambulia milioni 86 tu.
Malipo hayo yanatokana na utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 iliyorekebishwa mwaka 2008, ambayo inazitaka kampuni kama PAT kulipa tozo ya kodi ya huduma kwa halmashauri ya wilaya wanakofanyia shughuli zao kwa kiasi cha asilimia 0.3 ya faida wanayopata katika kila robo ya mwaka wa fedha.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Raymond Ndumbaro, ambaye alikuwa ofisini pamoja na Ofisa Mipango, Erick Mkinda, Ofisa Utumishi, Hemed Mwasimba na Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, ndiye aliyeithibitishia NIPASHE kuwa walianza kupokea ‘service levy’ ya gesi Aprili, 2012; maelezo yaliyofanana na yale yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ali Mohamed Mtopa na pia Mwanasheria wao, Godfrey Jaffari.
Taarifa inaonyesha kuwa malipo yaliyolipwa na PAT ni kama ifuatavyo:
Sh. 87,212,532 (Aprili 14, 2012), Sh. 42,377,600 (Mei 31, 2012), Sh. 88,832,164 (Agosti 10, 2012), Sh. 109,552,692 (Oktoba 31, 2012), Sh. 200,000,000 (Novemba 31, 2012), Sh. 200,000,000 (Januari 18, 2013), Sh. 121,389,513 (Februari 1, 2013), Sh. 114,631,241 (Mei 14, 2013), Sh. 164,284,208.21 (Juni 17, 2013) na kiasi hicho hicho cha fedha kikalipwa tena siku hiyo ya Juni 17,2013, yaani Sh. 164,284,208.21.
Malipo mengine yakafanyika Julai 31, 2013 (Sh. 117,076,055) na Oktoba 31, 2013, PAT wakalipa Sh. 139,793,184.
Kwa ujumla wake, hadi kufikia Desemba, fedha hizi za ‘service levy’ kwa wilaya ya Kilwa zikafikia Sh. 1,549,433,397.42
MGAWO WA SONGOSONGO
Hata hivyo, licha ya kuanza kulipwa kwa fedha hizo Aprili, kijiji cha Songosongo kilianza kupata mgawo wake wa asilimia 20 ya fedha hizo miezi mitano baadaye kama ifuatavyo:
Septemba 5, 2012 (Sh. 17,766,433), Novemba 22, 2012 (Sh. 21,800,000), Aprili 17, 2013 (Sh. 24,200,000) na Juni 28, 2013 wakapokea Sh. 23,114,689.
Nyaraka za Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Songosongo, Juma Hemed Mchenga, zinaonyesha kuwa walilipwa fedha hizo na DED wa Kilwa na kuziingiza kwenye akaunti yao namba 7012500020 iitwayo ‘Kijiji cha Ujamaa cha Songosongo’, benki ya NMB, Tawi la Kilwa Masoko.
Namba za stakabadhi za malipo ya DED zilikuwa 201201 ya Novemba 22, 2012, namba 201202 ya Aprili, 2013, namba 201203 ya Juni, 2013 na namba 201204 ya Novemba, 2013.
Mara zote, fedha hizo zilitambulishwa kama “20% ya Ushuru wa Gesi”.
Jumla ya fedha hizo zilizolipwa na DED kwa kijiji cha Songosongo ni Sh. 86,881,122, sawa na asilimia 5.6 tu ya ‘service levy’ yote iliyolipwa kuanzia Aprili, 2012 na wala siyo asilimia 20 kama ilivyopaswa kuwa, yaani Sh.309,886,679.484.
Hesabu hizo zinamaanisha kuwa Songosongo wamepunjwa jumla ya Sh. 223,005,557.484. Fedha hizo wangezipata zingesaidia shughuli zao za maendeleo hivyo kupiga teke umasikini kwa kiwango kikubwa.
Aidha, kiasi hiki ni mbali na mgawo mwingine wa Sh. milioni 40 (asilimia 20 ya Sh. milioni 200) zinazodaiwa kulipwa kimakosa kwa manispaa isiyokuwa ya mkoa wao wa Lindi.
Alipoulizwa kuhusiana na madai ya kupunjwa kwa malipo ya ‘service levy’ ya gesi kwa kijiji cha Songosongo, DED wa Wilaya ya Kilwa, Ado Mapunda, hakuwa tayari kueleza kiundani juu ya suala hilo.
"Tulishakubaliana kulipa katika quarter hizo (robo ya mwaka wa fedha)," alisema Mapunda wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu saa 12:13 jioni Alhamisi Januari 16, 2014.
Alipoulizwa zaidi kuhusiana na sababu za kupeleka kiasi kidogo tu cha tozo la gesi kwenye Kijiji cha Songosongo, tena kuanzia Septemba 5, 2012 ilhali wao walishaanza kupokea malipo hayo Aprili 14, 2012, Mapunda alisema kuwa anaweza kutoa ufafanuzi zaidi atakapokutana na mwandishi ana kwa ana na ikibidi hilo lifanyike Januari 25 wakati atakapokuwa Dar es Salaam kuhudhuria mkutano.
"Subiri hadi tarehe 25 nitakapokuja Dar (Dar es Salaam)... kwanza hapo hakuna habari yoyote, nishazungumza na waandishi wenzako wengi tu... nashangaa bado unaulizia suala hili. Hapo hakuna habari," alisema Mapunda.
Kisha akaelezea shaka yake kwa mwandishi kwa kusema:"Kwanza najuaje kama kweli nazungumza na mwandishi... hatujawahi kuonana. Hata kitambulisho chako sijakiona."
Alipoulizwa kama yuko tayari kuonana na mwandishi hata kesho yake (Ijumaa, Juni 17, 2014) ili aonyeshwe kitambulisho na kisha atoe huo ufafanuzi kuhusu ‘service levy’, Mapunda alikataa na kumsisitiza mwandishi kuwa asubiri hadi Januari 25, mwaka huu.
JANUARI 23
Alhamisi ya Januari 23, 2014, siku moja kabla ya kufikia siku ya ahadi ya kuonana na DED Mapunda, mwandishi alimpigia simu (Mapunda) na kumkumbusha kuhusu ahadi yake ya kutoa ufafanuzi wa malipo ya asilimia 20 yanayokwenda Songosongo wakati atakapofika Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mapunda alisema kuwa safari yake ya Dar es Salaam haipo tena na hivyo akamtaka mwandishi kwenda Kilwa Jumanne (Januari 28) ili akapate ufafanuzi huo.Mazungumzo kwenye simu yalifanyika kuanzia saa 7:33 mchana.
Katika mazungumzo hayo, DED alimshirikisha pia Diwani wa Kata ya Mitole ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Rafih Hassan Kuchao.
Wote walimtaka mwandishi afike Kilwa Jumanne.
Hata hivyo, saa moja baadaye (saa 8:33 mchana), mwandishi alimpigia simu DED (Mapunda) na kumtaarifu juu ya msimamo wake mpya; kwamba hatafika Kilwa Jumanne kama walivyokubaliana awali na hivyo, ampatie majibu kuhusiana na jambo moja tu, ambalo ni sababu za ofisi yake kulipa kiasi pungufu katika asilimia 20 ya ‘service levy’ kwa kijiji cha Songosongo kama inavyotakiwa kisheria.
Mara hii Mapunda aliamua kujibu. Akasema ni kweli wanalipa asilimia 20 kwa Songosongo na kwamba hadi sasa, kiasi walichowalipa ni sahihi. Akaongeza kuwa hadi kufikia Desemba, jumla ya kiasi walichowalipa ni takriban Sh. milioni 87.
Mwandishi alimtaka DED Mapunda ataje jumla ya fedha walizolipwa na PAT kuanzia Aprili, 2012 hadi Desemba, 2013, ili hatimaye kujua ni kwa namna gani asilimia 20 yake inatengeneza kiasi hicho cha Sh. milioni 87 anachodai kuwa ndiyo sahihi.
DED Mapunda alisema kuwa inahitaji muda kwani siyo rahisi kufanya ‘reconciliation’ ya fedha zote walizolipwa kupitia mazungumzo ya simu. Isitoshe, akakana kuwapo kwa manispaa inayodaiwa fedha za ‘service levy’ na halmashauri ya wilaya yao.
NIPASHE ilimuomba DED Mapunda ajumlishe malipo hayo yote na kutuma kiwango walichopata kupitia njia yoyote rahisi kwake, ikiwamo ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, au kumpigia simu kabisa mwandishi au hata kwa ‘kumbeep’ ili apigiwe na kumtajia kiasi hicho cha fedha kwa mdomo.
Hata hivyo, pamoja na maombi hayo NIPASHE ilimsisitiza kuwa hesabu ilizo nazo, ambazo zinaonyesha kuwa tayari wameshalipwa na PAT jumla ya Sh. bilioni 1.549 hadi kufikia Desemba 2013 hazijatoka kwingine kokote bali katika ofisi yake.
Pia gazeti lilimweleza kuwa kiasi hicho kimethibitishwa wakati wa mazungumzo ya pamoja baina ya mwandishi na Kaimu Mkurugenzi (Ndumbaro), Ofisa Mipango (Erick), na pia mweka hazina wao.
Mazungumzo baina ya mwandishi wa NIPASHE na viongozi hao wa halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuhusiana na ‘service levy’ yalifanyika mchana wa Jumanne ya Desemba 24, 2013, wakati huo Mapunda akiwa katika mapumziko ya krismasi.
Hadi tunakwenda mitamboni jana, DED Mapunda hakutoa mchanganuo wa fedha zozote wanazopeleka Songosongo.
AFISA MTENDAJI, WAZIRI TAMISEMI
Awali, walipoulizwa kwa nyakati tofauti kuhusiana na sababu za kutolipwa asilimia 20 ya fedha zote zitokanazo na ‘service levy’ ya gesi inayovunwa kijijini kwao, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Songosongo, Shamte Said Bungara na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Mchange, walistushwa na taarifa hiyo na kusema kuwa hawajui kuwa kiasi walichopata siyo asilimia 20 ya fedha zote zilizolipwa.
"Sisi tunachojua ni kwamba tunalipwa fedha zinazostahili... na hizi ndizo fedha ninazozitambua mimi (Sh. milioni 86), na risiti zake tunazo," alisema Mchange.
"Tena fedha hizi zinatusaidia sana... tumechukua sehemu na kukamilishia nyumba ya daktari wa kituo chetu cha afya cha Songosongo, fedha nyingine zimekuwa zikitusaidia pia kwa kulipa posho za vikao. Hadi sasa, benki tuna akiba ya zaidi ya Sh. milioni 79," aliongeza Mchange.
Ofisa Mtendaji Bungara alisema: "Binafsi siwezi kuzungumzia kitu nisichokifahamu vizuri... fedha anazosema mwenzangu (Mchange) ndizo na mimi ninazozijua. Tunazipata na zinatusaidia kwa mambo mengi katika kata hii yenye kijiji hiki kimoja tu (cha Songosongo). Hivi karibuni kuna mradi wa kuimarisha miundombinu ya umeme katika kata yetu yote na Tanesco wamekadiria kuwa gharama zitafikia Sh. milioni 102. Ni fedha hizi hizi ndizo zinazotegemewa kukamilisha kazi hii."
Diwani wa Kata ya Kilanjelanje, Ali Mtotela, aliiambia NIPASHE kuwa anachojua yeye na wenzake wengi ni kuwa asilimia 20 ya fedha za tozo la kodi ya huduma ya gesi hupelekwa Songosongo kila zinapolipwa kwani ndivyo sheria inavyotaka.
“Nitashangaa kusikia kuwa hawapewi kiasi hicho kadri inavyostahili kwa sababu mara zote tumekuwa tukiambiwa kuwa Songosongo wanalipwa kiasi hicho… nadhani ukimuuliza diwani wao atakuwa na majibu mazuri zaidi, ila wengi tunajua kuwa huwa wanalipwa kwa sababu ndivyo tunavyoambiwa kwenye vikao vyetu (vya Baraza la Madiwani Kilwa),” alisema Mtotela.
Diwani wa Kata ya Songosongo, Hassan Swalehe, alisema kuwa kwa taarifa alizo nazo, hadi sasa kijiji chao cha Songosongo kimeshalipwa takriban Sh. milioni 112 kutokana na mgawo wao utokanao na 'service levy' ya gesi; lakini akasema hafahamu kama kiasi hicho cha pesa walicholipwa ni kidogo na hakilingani na kile wanachostahili kukipata.
Mbunge wa Kilwa Kusini, Saidi Bungara, alistushwa vilevile kuhusu kuwapo kwa uwezekano wa kijiji cha Songosongo kutopewa mgawo wao wa ‘service levy’ kwa usahihi.
"Nitalifuatilia jambo hili kwa kina katika halmashauri yetu," alisema Bungara.
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa, alisema kuwa malipo ya ‘service levy’ yapo kisheria na kwamba, lolote kuhusiana na mgawo na matumizi yake hutokana na sheria ndogondogo za halmashauri husika na pia maamuzi ya Baraza la Madiwani.
“Kama kweli yapo makubaliano kuwa Songosongo walipwe asilimia 20 ya kodi hiyo (service levy) na kisha hawalipwi, basi hapo kutakuwa na tatizo… tutafuatilia,” alisema Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na NIPASHE kisiwani Songosongo umebaini kuwa baadhi ya viongozi wa kijiji hicho na wakazi wake wengi hawafahamu kiundani kuhusu mgawo wa ‘service levy’ unaopaswa kupelekwa kwao kutokana na huduma mbalimbali wanazozipata moja kwa moja kutoka kwa wawekezaji, kampuni ya PAT.
NIPASHE ilibaini kuwa wengi wa wakazi wa Songosongo, huridhishwa na huduma wanazopata kutoka PAT na kuamini kuwa hicho ndicho wanachokistahili.
Miongoni mwa faida wanazozipata sasa na kujikuta wakiacha kuhoji kuhusu fedha za ‘service levy’, kiasi wanachopata na namna kinavyotumika, ni pamoja na umeme wa bure kwa kila nyumba, maji ya bure wanayopewa na PAT kiasi cha lita 30,000 kila uchao, usafiri wa ndege bure kwa kila mmoja anayetaka kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam na pia kusomeshwa kila mwaka kwa watoto wao 10 bora wanaomaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi Songosongo.
Hawa husomeshwa na PAT katika Shule ya Sekondari Makongo ya jijini Dar es Salaam ambapo hadi sasa kuna wanafunzi 39 na kila mmoja hugharimiwa ada ya zaidi ya Sh. milioni 1.5 kwa mwaka, achilia mbali gharama za usafiri, vitabu, kalamu na madaftari ambazo zote hugharimiwa na wawekezaji.
“Kuna mengi mazuri tunayapata kupitia mradi huu wa gesi. Wadogo zetu wanasomeshwa bure, tunapewa maji bure, umeme bure, usafiri wa ndege bure na vingine vingi tu. Hakuna anayeuliza hayo mambo ya mgawo wa kodi kwa kijiji chetu,” alisema Selemani Said, mmoja wa wakazi wa Songosongo ambaye hujishughulisha na uvuvi wa pweza na kamba.
"Kama kuna fedha zinatolewa kwa kijiji chetu basi zitumike kusaidia ujenzi wa bandari yetu... pale (bandarini Songosongo) hali siyo nzuri sana. Sehemu ya kupumzikia abiria ni ndogo na hata choo hakuna kwa wasafiri wanaokwenda Kivinje," alisema Mwatime Hamad 'Mama Salma', mkazi wa eneo la Funguni kisiwani Songosongo ambaye ni mama lishe.
*Habari hii imekamilika kwa ufadhili wa TMF.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment