Home » » Swahiba wa Zitto atimkia CCM

Swahiba wa Zitto atimkia CCM

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Lindi ambaye hivi karibuni alitangaza kuachia wadhifa huo, Ali Chitanda, ametangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alifikia uamuzi huo juzi kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM za udiwani wa Kata ya Namikango, Wilaya ya Nachingwea.
Alisema licha ya kuamua kuhamia CCM, pia aliahidi kukifanyia chama hicho kampeni katika mikutano yake yote itakayoifanya wakati wa kampeni iliyoizindua hadi atakapohakikisha kiti hicho cha udiwani kinarejea CCM.
"Nimekuwa kwenye vyama vya upinzani kwa miaka mingi lakini tatizo la CHADEMA kinaendeshwa kama kampuni ya mtu binafsi inayojali masilahi ya viongozi wachache, hivyo ndugu zangu wananchi naomba msikiunge mkono chama ambacho hakifuati masilahi ya watu hasa maskini,” alisema Chitanda.
Akizungumza baada ya kutambulishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe, Chitanda aliwataka vijana wanaokimbilia CHADEMA kuanza kujiuliza kabla ya kufikia uamuzi wa kujiunga na chama hicho.
"Chama hicho kimepoteza mwelekeo kutokana na viongozi wachache kukifanya chama hicho kuwa ni taasisi binafsi," alisema amekitumikia kwa miaka 10, sasa ameamua kuondoka.
Aliongeza kuwa; “Kati ya watu ambao wamekaa muda mrefu na kushika nyadhifa mbalimbali kwenye vyama mbalimbali vya upinzani kuanzia NCCR-Mageuzi hadi CHADEMA, nimeamua kuachana na vyama hivyo baada ya kubaini kuwa ni mali ya wachache kwa masilahi yao.”
Kauli hiyo ya Chitanda iliungwa mkono na Akwilolmbe ambaye kabla ya kurejea CCM aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF na baadaye kuwa pia Naibu katibu mkuu wa CHADEMA na kuamua kuachana na vyama hivyo kwa kile alichosema kuchoshwa na vitendo vya ubinafsi. Chitanda inadaiwa alikuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Zitto Kabwe, ambaye hivi karibuni alivuliwa wadhifa huo.
Chitanda alitangaza kujiuzulu wadhifa wake mkoani Lindi siku chache mara baada ya Zitto, kuvuliwa wadhifa wake kutokana na kudaiwa kufanya uasi ndani ya chama hicho

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa