WANAKIJIJI cha Mirumba, Wilaya ya Kilwa, Lindi
walilazimika kufunga barabara kwa kupanga mawe na magogo baada ya watoto wawili
kugongwa na gari wakati wakivuka barabara na kusababisha kifo cha mmoja wao.
Watoto waliogongwa na gari aina ya Fuso ambalo
namba zake hazikupatikana ni Celina Anthony, aliyefariki dunia papo hapo na
Theresia Bernard, alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kitendo cha wanakijiji hao kufunga barabara
kilisababisha usumbufu ambapo abiria zaidi ya 1,000 walikwama kuendelea na
safari zao kwa zaidi ya saa nne.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho Musa Juma, Halima
Hassan, Mwajuma Saidi na Bakari walisema wameamua kufunga barabara ili kuishinikiza
serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuweka matuta kupunguza
ajali kijijini hapo.
“Ukweli tunateseka na barabara hii, tunahatarisha
maisha yetu wakati wa kuvuka barabara kwani magari yamekuwa yakikimbia mno wala
hawajui kama kuna kijiji wapunguze mwendo kwenye makazi ya watu, watoto wetu
wanagongwa na kufa wengine wanabaki walemavu lakini serikali ipo kimya na
tatizo hili ni la muda mrefu wanalijua,” walisema wanakijiji hao.
Suluhu ya vurugu hizo ilipatikana baada ya ombi la
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilwa, Yahya Mdogo, kuwataka wananchi hao kuwa na
subira huku akiwashauri kuondoa magogo na mawe ili magari yapite.
Rashid Mohamed na Ephrem Ndunguru, madereva wa
mabasi yaendayo mikoa ya Kusini mwa Tanzania walilalamikia kitendo cha askari
wa Usalama Barabarani kukaa msituni badala ya maeneo ya vijiji yenye msongamano
wa watu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George
Mwakajinga, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja watoto waliogongwa
kuwa ni Celina Anthony (7) aliyefariki dunia papo hapo na Theresia Bernard
alijeruhiwa.
Kamanda Mwakajinga alisema ajali hiyo ilitokea
Oktoba 4, mwaka huu saa tano asubuhi na kwamba dereva wa gari lililosababisha
ajali, Seif Ruanda, alijisalimisha Kituo cha Polisi Lindi kwa usalama wake.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment