Home » » Polisi jamii Lindi yahitaji kupatiwa elimu

Polisi jamii Lindi yahitaji kupatiwa elimu

Jeshi la polisi mkoani Lindi limetakiwa kutoa elimu ya polisi jamii
ili wananchi waweze kuwa na uelewa kuhusu kitengo hicho huku wakijua maana na dhamira yake halisi ili waweze kulinda amani na utulivu unaoendelea kumomonyoka hapa nchini.

Wito huo umetolewa na katika risala ya waendesha bodaboda wa kata ya nyangao, wilaya ya lindi vijijini mkoani humo katika sherehe za mapokezi ya vitambulisho vya polisi jamii na leseni za kuendeshea vyombo vya moto kwa vijana kumi na nane wanaounda kikundi hicho.

Mgeni rasmi katika sherehe hizo Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani Lindi kamishna msaidizi Renata Mzinga amewataka vijana hao kuwa watumiaji wazuri wa barabara na kuhakikisha kuwa ajali na vifo visivyo vya lazima vinakoma ikiwa ni pamoja na kupungua kwa wimbi la uhalifu.

Amesema kuwa dhana ya polisi jamii haikuanzishwa kwa bahati mbaya na kwamba polisi ni sehemu ya jamii na amewapongeza wananchi wa nyangao kwa kufikia hatua ya kujilinda wenyewe kwa ulinzi shirikishi na polisi jamii.

Naye mkuu wa polisi tarafa ya Mtama mkaguzi msaidizi Peter Msafiri amesema kuwa elimu ya polisi jamii iliyotolewa kwa kipindi kifupi imeleta mafanikio makubwa kwa wananchi kurudisha imani kwa jeshi lao na kushirikiana nalo katika kupambana na uhalifu.

Kundi hilo la waendesha bodaboda Nyangao lilianzishwa mwezi novemba mwaka jana likiwa na wanakikundi kumi na nane na baadae hadi kufikia thelathini na nane ambapo vijana kumi na nane waanzilishi wa kundi walipatiwa leseni hiyo ikiwa ni baada ya kupatiwa mafunzo ya miezi mitatu.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa