Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Waislamu nchini wametakiwa kutumia kipindi cha mfungo wa Ramadhani kuomba na kutubu dhambi zao pia kuwasaidia watu wasiojiweza ili wapate thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha viongozi wa dini mbalimbali mkoani Lindi.
Mama Kikwete alisema kuwa kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani ni kipindi cha kuomba na kutubu dhambi ili yule aliyefunga aweze kujiunganisha na Mwenyezi Mungu.
“Ibada na maombi yenu viendane na kutoka sadaka, wahudumieni watoto yatima, wagonjwa na watu wasiojiweza, muwe watu wa upendo kwani mahali penye upendo hakuna chuki, vita wala mafarakano”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kufuturu kwa pamoja na viongozi wa dini mbalimbali na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie funga ya heri na kuwazidishia huruma, upendo na mshikamano ndani ya mioyo yao.
Mama Kikwete pia aliwataka viongozi hao wa dini kuhubiri amani kwa waumini wao na kuhakikisha kuwa hawaipotezi amani kwa mambo yasiyo na tija kwani kuna nchi waliichezea amani na hivi sasa wanaishi kwa hofu na maisha ya vita.
“Mjitahidi kila mnapokuwa katika maeneo yenu ya ibada, sherehe na katika huzuni muhubiri juu ya kuwepo kwa amani kwani pamoja na umaskini wetu Tanzania tumejaliwa kuwa na amani kuna nchi ambazo ni matajiri lakini hawana amani na wananchi wake wanaishi maisha ya mashaka na hofu”, alisisita Mama Kikwete.
Kwa upande wake Shekhe na Kadhi mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani alimshukuru Mama Kikwete kwa ajili ya futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa kufunga ni moja kati ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na hiyo ni nguzo ya nne.
“Amri ya kufunga iliyotolewa na Mtume Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W) akiwa madina mwaka wa pili ndipo ilipoteremka amri hii hivyo basi waislamu wenye afya njema wanatakiwa kufunga”, alisema Shekhe Mushangani.
Aliendelea kusema kuwa mtu anayefunga na kuwa na hali ya kuamini na kutarajia thawabu anasamehewa makosa ya mwaka wote uliopita nyuma na mfungo mosi anaanza upya kuhesabiwa dhambi zake.
0 comments:
Post a Comment