Home » » Wananchi watakiwa kwenda kutibiwa hospitali na siyo kwa waganga wa jadi

Wananchi watakiwa kwenda kutibiwa hospitali na siyo kwa waganga wa jadiIMG_9356 
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akishiriki kucheza ngoma gogo inayochezwa na wananchi wa makabila mbalimbali mkoani Lindi wakati alipowasiri kwenye mkutano wa hadhara kwenye kata ya Matopeni wilayani Lindi Mjini tarehe 20.2.2013.
IMG_9380  Mke wa Rais na Mjumbe wa NEC ya Chama Cha Mapinduzi Mama Salma Kikwete akiwahutubia wananchi wa Kata ya Matopeni iliyoko Lindi Mjini tarehe 20.2.2013.
PICHA NA JOHN LUKUWI
……………………………………………..
Na Anna Nkinda, Maelezo  Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya ya Lindi mjini  kujenga mazoea ya kwenda hospitali kupima afya zao mara kwa  mara na kuachana na tabia ya kwenda kutibiwa kwa waganga wa jadi na kushikana uchawi kutokana na maradhi yanayowasumbua.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais alitoa rai hiyo  jana alipokuwa  akiongea kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Matopeni na Wailesi zilizopo wilaya ya Lindi mjini wakati wa ziara yake ya kichama ya siku saba katika wilaya ya Lindi mjini ya kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC.
Aliwasihi watu wenye tabia ya kutopenda kupima afya zao wakati wanaumwa na wale wenye tabia za kukimbilia kwa waganga wa jadi huku wakijua fika kuwa ni wagonjwa waache kwani wanaweza kupoteza maisha kwa magonjwa ambayo wangeweza kutibiwa katika vituo vya afya na kupona.
“Hakuna mtu asiyejua kuwa kuna Ugonjwa wa Ukimwi, muache suala la kushikana uchawi katika hili kwani ugonjwa huu haupatikani kwa kurogwa. Mtu mwenye virusi vya ukimwi  anapimwa  kinga za mwili za kupambana na magonjwa ( CD4) kama zipo chini atapewa dawa za kuongeza na akitumia dawa atakuwa na nguvu na kuweza kufanya kazi zake kama zamani jambo la muhimu asipitishe muda wa kuzitumia” , alisema Mama Kikwete.
Aidha Mjumbe huyo wa NEC alisema kuwa jamii nzima inahusika katika ulezi wa watoto lakini jambo la kusikitisha ni kuwa hivi sasa watu wamebadilisha mienendo ya maisha kila mtu anahangaika kulea mwanawe. Na kuwasihi wakazi wa Lindi kufuata maadili ya  zamani ya kuwalea watoto  kwani mtoto wa mwenzako ni wako .
“Ni jukumu la jamii nzima kuwalea watoto wao kwa kufuata  mila za kitanzania , wazazi ambao wakiambiwa kuwa watoto wao wanamienondo mibaya na kuja juu badala ya kuzifanyia kazi taarifa hizo waache tabia hiyo kwani watoto wakilelewa vizuri hata shuleni watakuwa na maadili mazuri na kuweza kufanya vizuri katika masomo yao”, alisema.
Kuhusu ufanyaji kazi kwa ushirikiano Mama Kikwete aliwataka wananchi hao kuachana na  mambo ya siasa kwani uchaguzi umeshapita hivyo basi wafanye kazi za maendeleo kwa na kujenga tabia ya kujitolea kufanya kazi.
Mama Kikwete alihoji,  “Hawa wazungu manaowaona wanakuja Lindi kufanya kazi wamekuja kujitolea ni jambo la muhimu kujitolea kufanya kazi za maendeleo, ukiambiwa kuna ujenzi wa shule, Zahanati wewe nenda ukajitolee usiseme ile si kazi ya Serikali sasa Serikali ni nani kama si wewe mwananchi?”.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2010 – 2015 Diwani wa kata ya Matopeni Suleiman Namkoma alisema kuwa idadi ya watoto wanaoanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka 45 hadi 60, kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la saba kutoka 20 hadi 43, kuongezeka kwa barabara zinazopitika kipindi cha masika na kiangazi na kuimarika kwa miundombinu na barabara za mifereji.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa