Home » » Wananchi watakiwa kwenda kutibiwa Hospitali na siyo kwa Waganga wa Jadi

Wananchi watakiwa kwenda kutibiwa Hospitali na siyo kwa Waganga wa Jadi



Na Anna Nkinda, 
Maelezo  Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa wilaya ya Lindi mjini  kujenga mazoea ya kwenda hospitali kupima afya zao mara kwa  mara na kuachana na tabia ya kwenda kutibiwa kwa waganga wa jadi na kushikana uchawi kutokana na maradhi yanayowasumbua.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais alitoa rai hiyo  jana alipokuwa  akiongea kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Matopeni na Wailesi zilizopo wilaya ya Lindi mjini wakati wa ziara yake ya kichama ya siku saba katika wilaya ya Lindi mjini ya kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC.
Aliwasihi watu wenye tabia ya kutopenda kupima afya zao wakati wanaumwa na wale wenye tabia za kukimbilia kwa waganga wa jadi huku wakijua fika kuwa ni wagonjwa waache kwani wanaweza kupoteza maisha kwa magonjwa ambayo wangeweza kutibiwa katika vituo vya afya na kupona.
“Hakuna mtu asiyejua kuwa kuna Ugonjwa wa Ukimwi, muache suala la kushikana uchawi katika hili kwani ugonjwa huu haupatikani kwa kurogwa. Mtu mwenye virusi vya ukimwi  anapimwa  kinga za mwili za kupambana na magonjwa ( CD4) kama zipo chini atapewa dawa za kuongeza na akitumia dawa atakuwa na nguvu na kuweza kufanya kazi zake kama zamani jambo la muhimu asipitishe muda wa kuzitumia” , alisema Mama Kikwete.


Aidha Mjumbe huyo wa NEC alisema kuwa jamii nzima inahusika katika ulezi wa watoto lakini jambo la kusikitisha ni kuwa hivi sasa watu wamebadilisha mienendo ya maisha kila mtu anahangaika kulea mwanawe. Na kuwasihi wakazi wa Lindi kufuata maadili ya  zamani ya kuwalea watoto  kwani mtoto wa mwenzako ni wako .
“Ni jukumu la jamii nzima kuwalea watoto wao kwa kufuata  mila za kitanzania , wazazi ambao wakiambiwa kuwa watoto wao wanamienondo mibaya na kuja juu badala ya kuzifanyia kazi taarifa hizo waache tabia hiyo kwani watoto wakilelewa vizuri hata shuleni watakuwa na maadili mazuri na kuweza kufanya vizuri katika masomo yao”, alisema.
Kuhusu ufanyaji kazi kwa ushirikiano Mama Kikwete aliwataka wananchi hao kuachana na  mambo ya siasa kwani uchaguzi umeshapita hivyo basi wafanye kazi za maendeleo kwa na kujenga tabia ya kujitolea kufanya kazi.
Mama Kikwete alihoji,  “Hawa wazungu manaowaona wanakuja Lindi kufanya kazi wamekuja kujitolea ni jambo la muhimu kujitolea kufanya kazi za maendeleo, ukiambiwa kuna ujenzi wa shule, Zahanati wewe nenda ukajitolee usiseme ile si kazi ya Serikali sasa Serikali ni nani kama si wewe mwananchi?”.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2010 – 2015 Diwani wa kata ya Matopeni Suleiman Namkoma alisema kuwa idadi ya watoto wanaoanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka 45 hadi 60, kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaofanya mtihani wa darasa la saba kutoka 20 hadi 43, kuongezeka kwa barabara zinazopitika kipindi cha masika na kiangazi na kuimarika kwa miundombinu na barabara za mifereji.
Namkoma alisema, “Tunakabiliwa na changamoto za uchache wa wataalam wa kada mbalimbali ngazi ya kata na jamii kukosa wataaluma wa huduma stahiki, ukosefu wa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa ngazi ya kata, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, kuchelewa kwa ruzuku ya Serikali kuu na makusanyo madogo ya Halmashauri na upungufu wa walimu wa shule ya msingi”.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mikumbi Zahara Suleiman alisema kuwa katika kata hiyo kuna vikundi vingi vya maendeleo lakini kwa mwaka 2010/2013 hakuna vikundi vilivyokopeshwa na Seambavyo ni  Ayayoli na Mafundi Seremali.
Suleiman alisema, “Tunawashukuru wafadhili waliovikopeshwa baadhi ya vikundi vyetu vya maendeleo kwani  kikundi cha Mwambao Fishing Group kilipewa na Mama Salma Kikwete boti na vifaa vya kuvulia vyenye thamani ya shilini milioni 57  na kikundi cha Uganda kilipewa pesa kutoka MACEP  shilingi milioni 15”.
Katika mkutano wa kata ya Mikumbi   Mjumbe huyo wa NEC aliwapokea vijana 18  waliokuwa wanachama wa CUF na kujiunga  na CCM. Akiwa katika kata za Matopeni, Wailesi  na Mikumbi alikabidhi  kadi  kwa wanachama  wapya wa CCM 43 , Umoja wa vijana 60, Umoja wa Wanawake  22 na Jumuia ya Wazazi  59.
Copyright 2007 ©MICHUZI JR

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa