Home » » MTANDAO USAMBAZAJI UMEME HAUJITOSHELEZI

MTANDAO USAMBAZAJI UMEME HAUJITOSHELEZI



na Hellen Ngoromera, Lindi
MTANDAO wa usambazaji umeme mkoani hapa umeelezwa kutotosheleza mahitaji hasa kwa makampuni makubwa yaliyoonyesha nia ya kuwekeza.
Hayo yalielezwa jana mjini hapa na Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoa, Charles Urio, wakati akizungumza na waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema kwa sasa mtandao huo unasambaza umeme wa KV 33 jambo ambalo ni changamoto kwao kwani tayari kiwanda cha kuzalisha saruji na wanga kimeshaonyesha nia ya kuwekeza mkoani hapa.
“Mfumo wetu wa kusambaza umeme hautoshelezi, hata hivyo tayari tumeshalipeleka suala hili ngazi za juu ili kulifanyia kazi. Hatutawaangusha wawekezaji kuendesha shughuli zao na katika kuliwezesha hili tutaanza kuipatia kampuni ya Starch umeme na baadaye kukiwezesha kiwanda cha saruji,” alisema Urio.
Akizungumzia mwamko wa mwananchi wa mkoa huo kujitokeza kupata punguzo la kuunganishiwa umeme kwa sh 99,000 badala ya sh 450,000, Urio alisema hatua hiyo imetoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kuunganishiwa umeme.
Alisema kuwepo kwa punguzo hilo kumeliwezesha shirika lake kupata wateja 100 kwa wiki jambo ambalo linatia matumaini ya idadi kubwa ya Watanzania wanaotumia umeme kuongezeka.
Kwa mujibu wa Urio mahitaji ya umeme kwa mkoa mzima yamefikia megawati 7. Alitoa hamasa kwa wananchi hao kujitoa kwa hali na mali kushiriki kwenye punguzo hilo ili waweze kupata umeme wa uhakika ili kuwainua kiuchumi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa