Home » » LINDI WACHEKELEA PUNGUZO LA UMEME

LINDI WACHEKELEA PUNGUZO LA UMEME



na Hellen Ngoromera, Lindi
MKOA wa Lindi umeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kutoa punguzo la bei ya kuunganisha umeme na kueleza hatua hiyo imewawezesha wananchi wake wengi kuichangamkia.
Hatua hiyo ilitangazwa juzi mjini hapa na Kaimu Mkuu wa mkoa, Regina Chonjo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
“Natoa pongezi kwa Wizara ya Nishati kwa kutambua kuwa nishati ya umeme ni muhimu katika maendeleo ya wananchi, hivyo kuamua kutoa punguzo la bei kwa kuunganisha umeme kwa sh 99,000 badala ya sh 450,000,” alisema Chonjo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea.
Alisema wananchi wa mkoa huo wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na uwezo mdogo kifedha, hatua ambayo ilisababisha wengi wao kushindwa kuuunganisha umeme kwa kiwango cha awali.
Pamoja na mambo mengine, alisema mkoa huo umejipanga vema kutumia nishati hiyo inayozalishwa kwa kutumia gesi na kwamba kwa sasa mkoa huo umekuwa kimbilio kwa wawekezaji kutokana na wengi kujitokeza kuwekeza.
Alitaja baadhi ya wawekezaji waliojitokeza kuonyesha nia ya kuwekeza mkoani hapa kuwa ni kampuni ya uchimbaji wa majini aina ya Nickel yaliyogundulika wilayani kwake (Nachingwea).
Alieleza pia kuwa kuingia kwa wawekezaji mkoani hapa kunatoa hamasa kwa wananchi kuharakishiwa maendeleo, kwani wengi wao wameipokea hali hiyo kwa uhalisia na wanaamini kwamba uwekezaji huo hasa kwenye gesi utabadili maisha yao.
Chanzo: Tanzania Daima





0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa