Home » » VIONGOZI WATAKIWA KUHOJI MATUMIZI FEDHA ZA CHF

VIONGOZI WATAKIWA KUHOJI MATUMIZI FEDHA ZA CHF

na Mwandishi wetu, Lindi
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeuomba uongozi wa Mkoa wa Lindi kuhakikisha unahoji na kusimamia matumizi ya fedha za tele kwa tele zinazolipwa na mfuko huo kwa halmashauri.
Fedha hizo ambazo zinalipwa na NHIF zinatakiwa kutumika katika ununuzi wa dawa na uboreshaji wa vituo vya kutolea matibabu, ili hatimaye kuondokana na mazingira duni ya kutolea huduma.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Meneja wa NHIF, Mkoa wa Lindi Fortunata Raymond, katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa ambacho kilijadili mambo mbalimbali ikiwemo taarifa ya utekelezaji ya mfuko huo ya mkoa.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Raymond alisema changamoto kubwa ambayo mfuko umekuwa ukipambana nayo ni fedha hizo kutotumika kama miongozo inavyotaka.
“Sisi kama mfuko tunaomba mtusaidie katika usimamizi wa fedha hizi ikiwemo kuhoji namna zinavyotumika…haiwezekani vituo viendelee kuwa na hali duni huku fedha zinazoweza kuviboresha zikitumiwa katika matumizi yasiyostahili,” alisema Raymond.
Alisema kama fedha hizo zitatumika kama ilivyoelekezwa, wananchi watapata huduma bora za matibabu.
Akijibu baadhi ya hoja, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Lodovick Mwananzila, aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa kufuata mwongozo uliopo.
Alisema hatasita kuchukua hatua kali kwa halmashauri itakayobainika kutumia fedha hizo kinyume na malengo yake.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa