Home » » MIL. 320/- ZA UFUTA KUIKOMBOA KILWA

MIL. 320/- ZA UFUTA KUIKOMBOA KILWA


na Happiness Mnale, Kilwa Lindi
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, imefanikiwa kukusanya sh milioni 320 kupitia ushuru wa zao la ufuta, fedha ambazo hazijawahi kufikiwa tangu zao hilo kuanza kulimwa.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la madiwani cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maendeleo ya wilaya hiyo, mkurugenzi mtendaji, Adoh Mapunda, alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na kubuni mfumo mpya wa ukusanyaji wa ushuru wa mazao ikiwamo kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani.
Aidha, Mapunda alisema kuwa changamoto nyingi zimejitokeza hasa katika suala la ushuru wa vijiji na ushuru wa ushirika ambapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakikwepa kulipa.
Akizungumzia kuhusiana na ushuru unaotokana na mauzo ya gesi, Mapunda alisema kuwa tayari wameshapata awamu ya kwanza sh milioni 87, na sasa wanasubiri awamu ya pili ambapo kibali kikipatikana kutoka Hazina watalipwa sh milioni 600.
Mapunda pia alisema kuwa fedha hizo za gesi walitakiwa kulipwa tangu mwaka 2008 hadi 2011 lakini kutokana na urasimu wa watendaji wa Hazina kudai uhalali wa wilaya hiyo kupata fedha hizo ndiyo chanzo cha ucheleweshaji.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa