Home » » Jaji Mkuu asema: una haja ya kufungua Mahakama Kuu Kanda ya Lindi

Jaji Mkuu asema: una haja ya kufungua Mahakama Kuu Kanda ya Lindi


Jaji Mkuu wa Tanzaniam,Mh. Mohamed Chande
           NA MARY GWERA, MAHAKAMA YA TANZANIA

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amesema kuwa kuna haja ya kufungua Mahakama Kuu Kanda ya Lindi ili kutoa nafasi kwa wananchi wa mkoa huo kupata haki zao kwa ukaribu zaidi.

Hayo yalisemwa na Jaji Mkuu hivi karibuni katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea Mahakama zilizopo mkoani Mtwara pamoja na Lindi.

“Kuna haja ya kimsingi kabisa kuanzisha Mahakama Kuu katika Mkoa huu ambao wananchi wake wanapata shida kipindi ambacho wanatafuta haki zao katika ngazi ya Mahakama Kuu,” alisema Mhe. Chande.

Aliongeza kuwa, wananchi wa mkoa huu wanasafiri masafa marefu zaidi ya kilometa 100 kutafuta haki zao katika Mahakama Kuu iliyopo mkoani Mtwara.

“Hali kama hii, si kwa mkoa huu pekee, kuna mifano mingine kadhaa ya mikoa ambayo wananchi wake husafiri katika mikoa mingine kutafuta haki, kama ilivyo kwa wananchi wa mkoani Kigoma ambao huudumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora,” aliongeza Jaji Mkuu.

Hata hivyo Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza kuwa, dira ya Mahakama ya Tanzania, ni kujenga Mahakama za ngazi zote katika kila mkoa ili kuwapa fursa wananchi kupata haki zao kwa wakati na kwa urahisi zaidi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Mkuu aliwapa changamoto Mahakimu wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kutenda haki kwa usawa bila kujali itikadi ya mtu.

“Ni jukumu la kila Hakimu kuwa na mikakati maalumu ya kumaliza kesi kwa wakati, hali ambayo itasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri na pia mlundikano wa Mahabusu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi Kanda ya Mtwara, Mhe. Shaaban Lila alisema kuwa kanda yake inakabiliwa na uchache wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo hali ambayo hupelekea baadhi ya vituo vya Mahakama visivyo na Mahakimu kutembelewa na Mahakimu wachache waliopo katika vituo vingine.

“Mhe. Jaji Mkuu nachukua fursa hii kuomba kuongezewa Mahakimu katika Kanda hii ya Mtwara ili kukidhi mahitaji ya utoaji haki kwa wananchi,” alisema, Jaji Lila.

Hata hivyo; Mhe Jaji Mkuu alibainisha kuwa katika ajira 300 za Mahakimu zilizotangazwa hivi karibuni, Kanda ya Mtwara na Lindi inatarajia kupata jumla ya Mahakimu 30.

Nafasi zilizotangazwa kwa Kanda hiyo ni kama ifuatavyo; Mtwara, Mahakimu 5, Masasi Mahakimu 3, Newala Mahakimu 2, Tandahimba Mahakimu 2, Lindi Mahakimu 4.

Nyingine ni Nachingwea Mahakimu 3, Liwale Mahakimu 2, Ruangwa Mahakimu 4 na Kilwa Mahakimu 5.

Ziara hiyo ya wiki moja imeazimia kuboresha mfumo wa utoaji haki ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Mahakimu, kuboresha na kuongeza miundombinu ya kutendea kazi ikiwa ni pamoja na majengo ya Mahakama na vifaa vya kufanyia kazi.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa