Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwasili
kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kwa ajili
ya kuembelea kampuni ya Universal Mining Ltd kujionea hali ya uzalishaji wa
jasi (Gypsum) unavyoendelea wakati wa ziara ya Siku tatu katika Mkoa wa Lindi
na Mtwara, Leo 17 Januari 2018. Picha Zote
Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akikagua uzalishaji wa madini aina ya Jasi
(Gypusm) katika kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani
Lindi, Leo 17 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akizungumzia umuhimu wa wachimbaji wadogo kuwa
na umoja ili kukuza ufanisi na tija katika kupanga bei ya rasilimali
wanazozalisha wakati alipozuru kijiji cha Hoteli Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya
ya Kilwa Mkoani Lindi, Leo 17 Januari 2018.
Na Mathias Canal, Lindi
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Leo 17
Januari 2018 amewataka wachimbaji wadogo wa madini Jasi(Gypsum) kuwa na umoja
na mshikamano katika uuzaji madini hayo na kuwa na kauli moja katika ushiriki
wa soko la bidhaa hiyo.
Mhe Biteko ameyasema hayo alipotembelea katika kijiji cha Hoteli
Tatu, Kata ya Mandawa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wakati wa ziara ya Siku tatu
katika Mkoa wa Lindi na Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na
makundi ya wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kuzitafutia
ufumbuzi.
Alisema kuwa kila mchimbaji anajipangia gharama aitakayo yeye
pasina kushirikiana na wachimbaji wengine ili kuwa na bei moja ambayo itakuwa
na tija na manufaa kwa kila mmoja hivyo kupitia umoja wao watakuwa na kauli na
maamuzi ya pamoja yenye tija na faida kwao.
Mhe Biteko aliwashauri wachimbaji hao kuwa na umoja utakaokuwa
na uwezo wa kudai bei itakayofanana kwa wote pia kuwa na uwezo wa kutengeneza
sheria ndogondogo ambazo zitatumika kujisimamia wao wenyewe.
Aidha, amezitaja Changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi
sambamba na wachimbaji wadogo hususani ubovu wa barabara ambapo ameishauri
Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kusaidia utengenezaji wa
Barabara itakayorahisisha usafirishaji wa jasi (Gypusm) na kurahisisha huduma
za wananchi ili kufika kwa urahisi katika Barabara kuu.
Mhe Biteko alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais
Dkt John Pombe Magufuli itaendelea na juhudi zake za kuweka miundombinu rafiki
kwa ajili ya wananchi, wawekezaji, na wachimbaji (wakubwa na wadogo) hivyo ili
kufikia adhma ya mafanikio hayo ni lazima kusema na kutekeleza maelekezo yote
ili kupiga hatua za maendeleo.
Alibainisha kuwa nia ya sekta ya madini ni kufanya mchakato wa
kuongeza pato la Taifa kufikia asilimia 10% tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo
sekta ya madini inachangia kiasi kidogo kwenye pato la Taifa.
0 comments:
Post a Comment