WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Lindi na wana-Ruangwa watumie fursa
zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la
Maulid Kitaifa mwaka huu.
Ametoa
wito huo leo (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na viongozi
wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya
kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri
Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid
na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3
asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Aliwataka
wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za
kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja
anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.
“Kwa
niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la
Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani
kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe
hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema.
Alisema
uamuzi huo wa BAKWATA ulitangazwa kwenye Baraza la Maulid lililofanyika
Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua kuadhimisha sherehe hizo kwenye
ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao makuu kila mwaka.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi hao kwamba maandalizi
yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa
ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia
vimekwishapatikana.
“Ninaomba
Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si
la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa
sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,”
alisema.
Alisema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa na mahubiri ya viongozi wa dini.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed
Mtopa alisema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa.
“Tunakuhakikishia wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa
Mufti waliopo hapa kwamba tumepokea hiyo heshima,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Itifaki kutoka BAKWATA Makao Makuu na Msimamizi wa Malidi
za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye alisema wana Ruangwa an wana
Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe hizo.
“Hamasa
haitatoka Morogoro au Dar es Salaam bali hapahapa Lindi. Tunataraji
watu wasiopungua 10,000 watahudhuria sherehe hizi za Maulid kutoka
wilaya zote za mkoa wa Lindi na hii ni mbali wawakilishi kutoka kila
mkoa wapatao 100 -150,” alisema.
Waziri Mkuu anatembelea vijiji vya jimboni mwake ambako atahutubia wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, NOVEMBA 5, 2017.
0 comments:
Post a Comment