Benny Mwaipaja, WFM,
Kampuni
moja ya Ujerumani ya Ferrostaal, inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha
mbolea katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kitakacho gharimu zaidi ya
Euro Bilioni 1 nukta 2 (1.2bln) ambacho kinatajwa kuwa kitakuwa moja ya
viwanda vikubwa vya mbolea Barani Afrika.
Hayo
yamesemwa na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, EGON KOCHANKE, wakati
alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, Jijini Dar es salaam, ambapo wawili hao wamezungumzia
masuala kadha wa kadha yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani
uliodumu kwa muda mrefu.
Balozi
Kochanke amesema kuwa kiwanda hicho kitakachojengwa kwa ubia kati ya
kampuni hiyo ya Ujerumani na wawekezaji wazawa na wengine kutoka Bara la
Asia, inatokana na hamasa kubwa ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda.
“Kiwanda
hiki kitakuwa kikubwa zaidi ya mara mbili ya kiwanda cha saruji cha
Dangote kilichoko Mtwara na kitagharimu Euro Bilioni 1.2, kitasisimua
uchumi wa nchi pamoja na kukuza ajira” alisema balozi huyo aliyeambatana
na naibu Balozi wa Ujerumani hapa nchini, John Reyels na Mkurugenzi wa
Ushirikiano wa nchi hiyo Julia Hannig.
“Mbali
ya Kampuni hiyo ya Ferrostaal, wawekezaji wengine ni kampuni ya Mbolea
ya Minjingu, na kampuni nyingine kutoka Pakistan ambayo kwa pamoja
wameingia ubia wa kujenga kiwanda hicho cha mbolea kitakachokuwa
uwekezaji mkubwa” Aliongeza Balozi Egon Kochanke.
Egon
Kochanke, ameiomba serikali kutatua changamoto ya gharama za gesi ili
kiwanda hicho kiweze kuanza ujenzi wake mapema iwezekanavyo na kuchochea
maendeleo ya kilimo hapa nchini.
Ameyataja
maeneo mengine ambayo nchi yake itaelekeza rasilimali zake kuwa ni
kuendeleza sekta ya afya, wajasiriamali wadogowadogo, sekta ya ufundi
mchundo pamoja na kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja
kuwekeza viwanda na biashara mbalimbali hapa nchini.
Aidha,
Balozi huyo wa Ujerumani ameahidi kuwa nchi yake iko tayari kutoa kiasi
kikubwa cha fedha ili kuifanyia ukarabati meli ya MV Liemba, inayofanya
zafari zake katika ziwa Tanganyika, ambayo ni meli ya kihistoria kwa
kuwa na umri wa zaidi ya miaka 100, ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa
watanzania na nchi jirani za Zambia, Burundi na DRC Kongo.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru
Ujerumani kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na
kwamba Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano huo.
Amesema
kuwa uwekezaji wa kiwanda kikubwa na cha mfano cha mbolea huko mkoani
Lindi, utachochea sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75
ya watanzania, kwa kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya wakulima na
mbolea ya ziada itauzwa nchi za nje.
Dkt.
Mpango, amemshukuru Balozi huyo wa Ujerumani kwa ahadi yake ya kusaidia
kukarabati meli ya MV Liemba, na kiomba nchi hiyo kusaidia ununuzi wa
meli mpya ili kuimarisha usafiri na usafirisha wa watu na mizigo katika
eneo la maziwa makuu.
Vilevile
ameiomba nchi hiyo kuendeleza misaada yake katika sekta ya ufundi
kupitia mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta) pamoja na kuendelea kutoa
ufadhili wa masomo ya juu kwa wanafunzi wa kitanzania kwenda kusoma
nchini humo kama ambavyo imekuwa ikifanya miaka mingi iliyopita kupitia
Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Balozi
Kochanke amekubali kufanya hivyo na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari
kushirikiana na Tanzania katika mambo hayo na masuala mengine, ikiwemo
kuishauri namna bora ya kuhamishia Serikali mkoani Dodoma, wakitumia
uzoefu wa nchi hiyo ilipohamisha makao makuu yake kutoka Berlin kwenda
Born.
0 comments:
Post a Comment