Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Anna
Nkinda – Johannesburg, Afrika ya Kusini
15/06/2015
Asilimia 73 ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) yanayotokea miongoni
mwa vijana Barani Afrika huwapata wasichana huku asilimia 15 ya vijana
wote ndiyo wanaotambua hadhi yao ya VVU
na hivyo kusababisha tatizo hilo kuendelea
kuwa kubwa.
Hayo
yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano
wa 15 wa Umoja wa wake wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi
(OAFLA) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Sandton Convention Centre
mjini Johannesburg Afrika ya Kusini.
Mama Kikwete
ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema tatizo
la VVU na Ukimwi bado ni kubwa miongoni mwa vijana wa kike na kama wataendelea
kuambukizwa kwa kiwango hicho kutakuwa na muda mrefu wa kupambana na maambukizi
kwa wenzao ambao hawajaambukizwa na kutahitajika muda mrefu wa matumizi ya dawa
za kufubaza VVU ambazo ni ghali.
“Ushauri
wangu kwenu ni kuongea juhudi zaidi ili kupaza sauti za watoto wetu wa kike
ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, kufanya mapambano dhidi ya
Ukimwi kuwa ni agenda ya kudumu ya OAFLA
kila tutakapotayarisha mipango yetu ya taarifa mapambano dhidi ya VVU ni muhimu
kujumuishwa”, alisisitiza Mama Kikwete.
Kwa upande wa elimu Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto wa kike kutafungua
fursa za kuweza kuboresha afya, kipato chake na hatimaye kujiongezea uwezo wake
binafsi na familia kwa ujumla.
Alisema, “Tunatambua
kwamba kwa kadri mtoto wa kike anavyokaa muda mwingi shuleni ndivyo anavyoweza
kuepuka uzazi katika umri mdogo, vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi na
umaskini”.
Mama Kikwete alisema ili
kukabiliana na changamoto hizo Taasisi ya
WAMA imeendesha kampeni ya mtoto
wa mwenzio ni mwanao;Mkinge na Ukimwi kwa njia za upashanaji habari, mafunzo na
uraghibishi kwa kutoa mafunzo ya stadi
za maisha na ujinsia kwa vijana wa rika mbalimbali ili kuwawezesha kuepuka
ujauzito na maambukizi ya VVU.
“Tumetekeleza afua
mbalimbali za kusaidia kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kutoka kwa Mama
Kwenda kwa mtoto (EMTCT), kushirikiana na jamii za wafugaji ili kuepuka desturi
zinazochochea vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi katika umri mdogo, tohara
kwa wasichana na unyanyasaji wa kijinsia na kutekeleza kampeni ya kupima na
kutibu mabadiliko ya awali ya saratani ya shingo ya kizazi”, alisema Mama
Kikwete.
Akiwakaribisha wake hao
wa Marais, Mke wa Rais wa Afrika ya Kusini Mama Thobeka Madiba Zuma alisema
muda umefika kwa wao kuonyesha majukumu
yao katika Bara la Afrika kwa kuungana kwa pamoja na viongozi wa jamii zao ili waweze
kuondoa unyanyasaji wa kijinsia kwa
wanawake zikiwemo mila kandamizi, kusimamia ili wanawake wapate haki za uchumi,
afya ya uzazi na kulinda haki za wazee,
walemavu na watoto.
“Vijana wapate elimu ya
afya ya uzazi huduma ya kuzuia
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ipatikane kwa urahisi
kwa wanawake walio na maambukizi hii itasaidia
wanawake kujifungua watoto wasio
na maambukizi na hivyo kutokuwa na maambukizi katika vizazi vijavyo”, alihimiza
Mama Thobeka.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS)
kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya kushughulikia Uchumi ya Afrika (ECA)
Rosemary Museminali alisema kama jamii itaamua kushirikiana na kufanya kazi kwa
pamoja ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja
na mashirika binafsi ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi inawezekana kwa kiasi
kikubwa kumaliza maambukizi ya VVU.
Rosemary alisema, “Katika nchi za Afrika msichana mmoja kati ya
wasichana 10 wenye umri wa chini ya miaka 15 ana mtoto, wasichana hawa wanatakiwa kuwa shule na kubeba vitabu na siyo kubeba watoto
pia wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU
Mkutano huo wa wake wa
marais wa Afrika ulienda sambamba na mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi na viongozi
wa Serikali wa Afrika uliomalizika leo
mjini Johannesburg.
0 comments:
Post a Comment