Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewaomba wananchi kuipigia kura ya ndiyo katiba
inayopendekezwa kwa kuwa ni bora na imezingatia mahitaji ya makundi yote ya
jamii.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa ombi hilo jana wakati akiongea na
wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika tawi la Mikumbi Magharibi kata ya Wailes wilayani humo.
Alisema katiba
inayopendekezwa ni ya watanzania wote na imegusa maeneo yote muhimu kwa ustawi
wa wananchi, inazungumzia haki za wanawake, wazee, wavuvi, watoto na watu wenye
mahitaji maalum.
“Katiba iliyopo sasa nayo
ni bora, lakini hii inayopendekezwa ni
bora zaidi kwani imezitaja haki za mwanamke, mtoto, kijana,mzee na watu
wenye mahitaji maalum lakini katika katiba hii ya sasa makundi haya hayatajwi. Msipoteze
nafasi, siku ikifika jitokezeni kwa
wingi mkaipigie kura ya ndiyo”, Mama Kikwete alisema.
MNEC huyo pia aliwahimiza
wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia kura katiba inayopendekezwa na kushiriki
katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu wa kumchagua Diwani,
Mbunge na Rais.
Alisisitiza, “Zoezi hili
la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura ni jipya, hata kama
unakitambulisho cha zamani ni lazima ukajiandikishe ili uweze kupata
kitambulisho kipya kwakuwa hicho cha zamani hakitatumika tena”,.
Kuhusu maambuki ya
Virusi Vya Ukimwi alisema ni tatizo na kuwasihi wananchi hao kujilinda na kutoruhusu ugonjwa huo usio na kinga wala tiba kuingia ndani ya nyumba zao.
“Hali ya maambukizi ya
ugonjwa wa Ukimwi katika nchi yetu inazidi kupungua kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka
2005 hadi kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka
2014, hadi sasa jumla ya wananchi
milioni 24 wamepima VVU kwa hiari.
“Kupima kwa hiari kutakusaidia
kujua kama unamaambukizi au la, na ikiwa utakuwa na maambukizi utatumia dawa
za kupunguza makali ya ugonjwa na kuchukua tahadhari ili usiwaambukize
wengine na kama hauna maambukizi utajikinga”, Mama Kikwete alisema.
Akiwasalimia wananchi
waliohudhuria mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza aliwasisitiza
wazazi na walezi kuona umuhimu wa kusimamia elimu ya watoto wao kwani wakisoma wataweza kuzitumia
fursa za kitaalam zinazopo mkoani humo.
Alisema hivi sasa shule
za msingi na Sekondari ziko nyingi lakini cha kushangaza kuna baadhi ya wazazi hawataki
kuwapeka watoto wao shule.
Mahiza alihimiza, “Kwa
yeyote anayejijua ana mtoto nyumbani ambaye amefaulu mtihani wa darasa la saba
na hataki kumpeleka shule ajiandae kwakuwa
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake, natoa angalizo ifikapo ijumaa ya wiki hii watoto hawa wawe shuleni kwani
elimu ni mkombozi wa maisha yao”, .
Katika mkutano huo wanachama wapya 202 walijiunga na Chama Cha Mapinduzi kati ya hao wawili walitoka Chama cha Wananchi
CUF.
Wakati huo huo MNEC Mama
Kikwete alitembelea kwa nyakati tofauti matawi
ya Mmongo, Majani Mapana na Mikumbi Magharibi na kuongea na viongozi wa Halmashauri kuu ya matawi mambo
mbalimbali yahusuyo chama hicho .
Aliwataka wajumbe
kuwahimiza wananchi wawe na utamaduni wa
kufuga kuku wa asili (kienyeji) kwa kila kaya kwa kufanya hivyo itawasaidia kukuza uchumi wao na familia zao
na hivyo kujikomboa kutoka maisha ya umaskini.
Mama Kikwete alisema
ufugaji wa kuku wa asili hauna gharama
kwani kuku mwenyewe anajitafutia chakula, mfugaji atakachompa ni mtama au pumba kidogo
na maji ya kunywa pia nyama yake ni tamu na haina madhara kiafya ukilinganisha
na kuku wa kisasa.
Alisema, “Ufugaji wa
kuku una faida licha ya kuwa ni kitoweo bali pia ni biashara, hivi sasa kuku mmoja anauzwa shilingi 12000 hadi 15000, ukiuza
mmoja ada ya shule itapatikana na mtoto atasoma na wewe mwenyewe utavaa. Jitahidini
kila kaya iwe na kuku japo 20”,.
Kwa upande wa ardhi
aliwasisitiza kutokubali kuuza maeneo
yao kiholela kwani maeneo mengi yako karibu na Bahari ya Hindi na thamani yake ni kubwa hivyo basi wayatunze
yatawasaidia katika siku zijazo .
Mama Kikwete yupo
wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za CCM ikiwa ni pamoja na kufanya
vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment