Na
Anna Nkinda – Maelezo
19/2/2015
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Serikali ya Japani wametiliana saini
mkataba wa mradi wa upanuzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo
Rufiji mkoani Pwani utakaogharimu shilingi milioni mia tisa.
Utiaji
saini wa mkataba huo umefanyika leo katika ofisi za WAMA zilizopo jijini
Dar es Salaama kati ya Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mama Salma Kikwete na Balozi
wa Japani nchini Masaki Okada.
Akiongea
mara baada ya kusaini makubaliano hayo Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuwajali watanzania na
kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha elimu.
Alisema
mradi huo utapanua na kuboresha uwezo wa shule kutoa huduma bora ya elimu
ambapo kutakuwa na upanuzi wa jengo la utawala kwa kuongeza ghorofa moja
ili kupata chumba cha walimu ambao wataweza kufanya mikutano yao, kituo cha
walimu, na maktaba.
Ujenzi
wa chumba maalum cha kompyuta ambacho kitawafanya wanafunzi kusoma somo hilo
kwa vitendo, uwekaji wa mitambo ya mawasiliano kwa ajili mtandao wa Internet
katika eneo la shule ambao haukuwepo shuleni hapo.
“Pia
ninawashukuru kwa msaada wa vitabu vya kiada na ziada ambavyo vitafika hivi
karibuni , elimu ni kitabu na ukisoma bila kitabu hutakuwa na mapana zaidi,
tukipata vitabu vya ziada vitasaidia kujenga ufahamu wa mtoto kuweza
kuchanganua mambo mbalimbali”, alisema Mama Kikwete.
Kwa
upande wake Balozi Okada alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili
ambazo ni ujenzi wa maabara ya kompyuta pamoja na kutoa vifaa muhimu na
kuunganisha Broadband Internet kwenye maabara.
Balozi
Okada alisema, “Baada ya mradi huu kukamilika sio tu wanafunzi wataweza
kujifunza kompyuta bali pia watatumia internet kupata taarifa nyingi na za
kisasa zinazopatikana mtandaoni.
“Sehemu
ya pili ni upanuzi wa jengo la utawala. Mradi huu ukikamilika wanafunzi
hawatapata tabu ya kutafuta walimu kwa ajili ya kuuliza maswali kuhusu masomo.
Ninaamini kwamba mazingira bora kwa walimu yanaboresha mazingira ya kusomea kwa
wanafunzi”.
Aidha
Balozi Okada alisema Hayao Nakayama ambaye ni mtu wa kwanza kutoa
ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ametoa zaidi ya milioni mia moja na
themanini ambazo zitatumika kwa ajili ya kununulia gari la dharura la
kubebea wagonjwa na maelfu ya vitabu ambavyo vitasafirishwa siku za karibuni
kutoka nchini Japani.
Balozi
huyo alisema vitabu hivyo siyo tu vya masomo ya sayansi na hisabati
vinavyohitajika kuongeza ujuzi lakini pia kuna vitabu vya kiingereza na kiswahili
kama vile hadithi, riwaya halisi pamoja na wasifu wa watu mashuhuri wanaume na
wanawake kutoka duniani kote ikiwamo Japani.
“Wanafunzi
watajifunza hadithi za mashujaa waliopigania elimu kwa wanawake na waasisi wa
kampuni kubwa kama vile Panasonic na Honda. Wataweza kupata watu wa mfano wa
kuigwa kati ya hao wataweza kujifunza kutokana na maisha yao jinsi
walivyotekeleza ndoto zao na kuishi siyo tu kwa ajili yao binafsi bali kwa
familia, marafiki na watu katika jamii na taifa kwa ujumla”, Balozi Okada
alisema.
Shule
ya Sekondari ya WAMA-Nakayama yenye wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza hadi
cha tano wengi wao wakiwa ni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira
hatarishi ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 na hadi sasa ina wanafunzi 366.
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment