Na Anna Nkinda – aliyekuwa
Lindi
Wananchi wa
mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya ndiyo katiba
inayopendekezwa kwani ni bora na imegusa maeneo yote kwa ajili ya maendeleo ya
Watanzania.
Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na wananchi waliohudhuria sherehe ya kushangilia ushindi wa uchaguzi
wa Serikali za mitaa katika mtaa wa Ruaha kata ya Mingoyo wilayani humo.
Katika uchaguzi wa
Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wananchi
wa mtaa wa Ruaha waliwachagua Mwenyekiti na wajumbe wote watano kutoka Chama
Cha Mapinduzi.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema katiba inayopendekezwa
imeangalia maeneo yote yanayomgusa binadamu ikiwa ni pamoja na haki za wanawake
na watoto, watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu na wazee.
“Katiba iliyopo sasa
ilitungwa na baadhi ya watu waliokuwa madarakani kwa wakati ule na haikuwahusisha
wananchi, lakini hii inayopendekezwa wananchi
wameshiriki kuitunga kwa kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Lindi Mwantumu Mahiza aliwahimiza wananchi hao kujiandikisha katika
daftari la kudumu la wapiga kura ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Mahiza alisema kama kuna
watu waliojiandikisha katika miaka ya nyuma wabebe vitambulisho vyao ili viweze kunukuliwa na kwa wale wenye umri
wa kuanzia miaka 18 wakajiandikishe na walio na umri wa chini ya hapo
wasijiandikishe.
Aliwaasa wananchi
hao kutokubali wageni waliokaa katika maeneo yao kwa kipindi cha chini ya miezi sita kujiandikisha.
Akisoma taarifa ya CCM
tawi la Ruaha Mohamedi Ngashona ambaye ni mjumbe alisema viongozi hao wamejipanga kutatua
changamoto zinazowakabili wananchi wa mtaa huo ambazo ni uharakishaji wa ujenzi
wa zahanati, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa nyumba za walimu.
Kuwatambua kaya maskini
na wazee kwa kuwapatia huduma muhimu, uimarishaji wa barabara ya kutoka
Mnazimmoja hadi Ruaha na utekelezaji wa sera ya umeme vijijini hasa vilivyopitiwa
na mradi wa bomba la gesi.
Katika mkutano huo
jumla ya wanachama 43 walijiunga na
chama hiyo kati yao wanne walitoka Chama cha Wananchi CUF .
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment