Home » » SHULE NNE ZAKOSA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA

SHULE NNE ZAKOSA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA

HUKU baadhi ya mikoa ikikabiliwa na changamoto ya wanafunzi kukosa nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, hali imekuwa tofauti kwa Mkoa wa Lindi, baada ya shule nne za sekondari kukosa wanafunzi wa kujiunga na shule hizo.
Akitoa taarifa ya maendeleo katika kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika jana mjini hapa, Ofisa Elimu Mkoa wa Lindi, Silas Samaluku, alisema mkoa huo una shule za sekondari 115, lakini kati ya hizo nne zimekosa wanafunzi wa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.

Alisema pamoja na hali hiyo, wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wamepangiwa shule, huku shule za Namapwia na Kilimarondo za wilayani Nachingwea, Madangwa wilayani Lindi na Nandanga wilayani Kilwa zikikosa wanafunzi.

“Wanafunzi 17,249, walisajiliwa kuhitimu elimu ya msingi kati ya hao wavulana ni 7,981 na wasichana 9,448, lakini kati yao waliofanya mtihani ni 16,682 na wasichana 9,150 sawa na asilimia 95.71.

“Wanafunzi waliofaulu na kupata alama 100 hadi 250, walikuwa 6,857 kati ya hao wavulana 3,644 na wasichana 3,213 sawa na asilimia 41.1 ambayo imepanda ukilinganishwa na mwaka 2012 ambapo ilikuwa asilimia 22.60,” alisema Samaluku.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili mfululizo, wanafunzi wa Wilaya ya Liwale wamefanikiwa kuongoza katika mitihani ya darasa la saba na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa.

“Mwaka 2013, Wilaya ya Liwale imeongoza kwa kufaulisha kwa asilimia 53.37, wilaya nyingine na asilimia zao kwenye mabano ni Nachingwea (50.05), Lindi Manispaa (42.42), Ruangwa (42.34), Kilwa (33.74) na Lindi Vijijini (31.45),” alisema.

Chanzo:Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa