Home » » TAMKO RASMI NA TAARIFA RASMI KUTOKA CHADEMA KUHUSU KUJIUZULU KWA KWA MWENYEKITI CHADEMA MKOA LINDI MJUMBE BARAZA KUU TAIFA BW ALLY OMARY CHITANDA

TAMKO RASMI NA TAARIFA RASMI KUTOKA CHADEMA KUHUSU KUJIUZULU KWA KWA MWENYEKITI CHADEMA MKOA LINDI MJUMBE BARAZA KUU TAIFA BW ALLY OMARY CHITANDA

 Kutokana na kuwepo kwa taarifa ya Ndugu A.O. Chitanda, huku pia waandishi
wa habari wakitaka kujua na kupata ukweli kutoka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA, tunapenda kutoa ufafanuzi mfupi;

Kwanza suala la maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi ndani ya chama,
Ndugu Zitto Kabwe na Dkt. Kitila Mkumbo, mjadala wake kwa upande wa chama
umeshafungwa, huku taratibu za kikatiba za ndani ya chama zikiendelea.

Pili suala la restructuring ya Makao Makuu ya Chama. Chitanda ametoa
taarifa akiwataja wakurugenzi wafuatao, kuwa ni wapya;
 
 *1. Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson.
*2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika (Mb).*
*3. Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji Mhe. Anthony Komu.
*4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema.
*5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.

 Wakurugenzi wote aliowataja si wapya. Mkurugenzi pekee ambaye uteuzi wake
ni mpya na umefanyika hivi karibuni na kuthibitishwa ni Mwanasheria Peter
Kibatala, atakayesimamia Kurugenzi ya Sheria na Haki za Binadamu.

Kama ni suala la kuangalia mtu anatokea wapi (ambalo halijawahi wala
haliwezi kuwa moja ya vigezo), ili kuonesha ukweli na kubainisha uongo wa
watu wanaojaribu kufanya kazi ya CCM wakisema wao ni wanCHADEMA, kwa
kutumia propaganda zile zile na kuzifanya kuwa ni kete zao za kisiasa,
tunaweza kutaja maeneo ya wanakotoka au asili yao kama ifuatavyo;

*Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji, Antony Komu- Kilimanjaro.

*Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare- Kagera.

*Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila- Dodoma.

*Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John John Mnyika- Mwanza

*Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema- Kilimanjar.

*Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala- Morogoro.

Hadi sasa uteuzi wa kurugenzi za Makao Makuu ya CHADEMA haujakamilika. Bado kuna nafasi zinazotakiwa kujazwa kwa kufuata taratibu za chama.

Hii ni kwa sababu *restructuring, *inayofanyika ndani ya chama, hadi sasa
inaendelea katika ngazi ya Makao Makuu na kanda, kisha itaendelea kwa ngazi
za mikoa, wilaya, majimbo, kata, kijiji na hatimaye kitongoji.

Katika restructuring hiyo ya nafasi za uteuzi, inayoendelea sasa ambayo
inakwenda hatua kwa hatua, hadi kuwa na makatibu wa kuajiriwa ngazi ya
chini ya chama, chama kinazingatia uwezo, uadilifu na utayari wa mtu katika
kutoa utumishi bora kwa wanaCHADEMA na Watanzania wote katika nafasi
husika.

Suala la maslahi ya watumishi wa CHADEMA ni utaratibu wa chama ambao
unajadiliwa, kufikiwa uamuzi na kisha kuridhiwa  kwenye vikao vya chama,
kama ilivyofanyika kwenye kikao cha Kamati Kuu kilichoketi karibuni.

Katika suala hili la maslahi ya watumishi wanaojitolea Makao Makuu ya
CHADEMA ambayo si siri, Ndugu Chitanda amesema uongo mkubwa. Kwanza si kweli kuwa Ofisa Mwandamizi anaweza kulipwa posho kubwa kuliko Mkurugenzi wa kurugenzi husika.

Ndugu huyo anadhihirisha uongo huo yeye mwenyewe kwa kuandika hivi; “
*800,000/=* za awali na sasa itakuwa ni kuanzia *Tshs. *
*1,500,000-2,500,000/=* kwa Mkurugenzi na kutoka *Tshs. **6,800,000/=* kwa Afisa Mwandamizi na sasa ni *Tshs.**1,000,000-1,500,000/=”
.*

Pia si kweli kuwa kila mtumishi anayejitolea Makao Makuu analipwa.
Mathalani, wakurugenzi wenye nafasi za ubunge, hawalipwi hata shilingi moja
kwa kazi zote wanazokitumikia chama na Watanzania kwa ujumla.

Kwa maelezo hayo ya kutengeneza, ni kwamba hadi sasa Ofisa Mwandamizi
anapokea posho kubwa kuliko Mkurugenzi na hata baada ya ‘restructuring’
atapata posho kulingana na Mkurugenzi. Anapaswa kuwa mkweli. Mtu anayetaka kuonekana muungwana, anapaswa kujiweka mbali na uongo pamoja, maneno ya kutunga pamoja na upotoshaji wa makusudi.

Kama ilivyoandikwa hapo juu, *restructuring* inaendelea. Ni hatua kwa
hatua. Itafika ngazi za chini kama Baraza Kuu lilivyoagiza. Kwa sababu hiyo
hadi sasa uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Wilaya haujafanyika.

Hata hivyo ruzuku imekuwa ikipelekwa kila kanda, mkoa, wilaya na jimbo kama
ilivyoridhiwa na Kamati Kuu. Na hii ni zaidi ya pikipiki, kompyuta na
magari yaliyopelekwa kila kanda. Angelikuwa mkweli, nagelisema na hili pia.


Ndugu Chitanda anajichanganya katika taarifa yake yote. Hii ni moja ya sifa
ya kukosa hoja hivyo mtu anaamua kuibua viroja au kutunga maneno kwa sababu ya kushindwa kusema ukweli.

Anaonesha kuwa alikuwa mtu aliyeaminiwa hadi kuwa katika vikao muhimu,
lakini wakati huo huo anasema kuna ubaguzi! Tunapaswa kumhurumia kwa
kushindwa kuunganisha hata mawazo yake na kupata mtiririko wa hoja zenye
mantiki! Angelikuwa mkweli angesema katika vikao vya sekretarieti na CC,
aliingiaje kama kuna ubaguzi wa dini!

Kwa sababu anazozijua yeye, Ndugu Chitanda ameamua kujipachika cheo ambacho hajawahi kuwa nacho. Amejiita kuwa ni Katibu wa Sekretarieti ya Makao Makuu. Ndani ya CHADEMA pamoja na kwamba nafasi hiyo imetajwa ndani ya Katiba ya Chama, hakuna mtu ambaye ameteuliwa kutumikia nafasi hiyo. Kama anaweza  athibitishe kwa kutoa barua ya uteuzi kutoka kwa Katibu Mkuu.

Mahali pengine amejitambulisha kuwa ni Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu. Ofisi
hiyo ina Katibu Mtendaji mmoja ambaye ni Mzee Victor Kimesera, mmoja wa
waasisi wa CHADEMA.

Operesheni ya Chama inayoendelea nchi nzima kwenye majimbo 103, si suala la
siri wala lengo bovu kama anavyotaka umma uamini. 

Ni mwendelezo wa mpango mkakati wa chama kupitia progamu za Vuguvugu la
Mabadiliko (M4C), unaotekelezwa kwa hatua mbalimbali na kwa mbinu tofauti
tofauti pamoja na dhana ya CHADEMA ni msingi.

Operesheni hiyo ambayo ni mwendelezo wa nyingi za namna hiyo zinazokwenda ngazi za chini kabisa za chama, zikilenga kuimarisha taasisi na mifumo, imeanza wiki hii na ilitangazwa mbele ya waandishi wa habari.

Tungependa kumalizia ufafanuzi huu mfupi kwa kutoa tahadhari kwa umma kuwa makini na matamko ya watu wa namna hii. Maana tunajua kwa uhakika yako mengi ya namna hii yatatokea kadri ambavyo Watanzania wanakaribia kuona na kuishi matumaini ya mabadiliko ya kiutawala na mfumo ndani ya nchi yao.

Mathalani katika taarifa yake, Ndugu Chitanda amedhihirisha na kuonesha
kuwa ni aina ya watu ambao wanaCHADEMA na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kuwaangalia kwa macho ya kuhoji na tahadhari ya hali ya juu, anasema hivi;

*“Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa Zitto Kabwe na Dkt Kitila
Mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao ni
kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda.”  

Aya hiyo pekee inayotumia lugha wanayotumia mahasimu wa CHADEMA,
wakiongozwa na viongozi waaandamizi wa CCM, wanaohangaika kutokana na
Watanzania kuwakataa, wakijiandaa kuwaondoa madarakani kwa sababu sera zao zimeshindwa, inatosha kuonesha uhalisia wa taarifa yake yote.

Ni kauli za namna hii (kuwatisha na kutaka kuwatenganisha  Watanzania)
ambazo zimekuwa zikitumiwa na watawala kama njia pekee ya kutaka kuzuia
upepo wa mabadiliko unaovuma nchi nzima, zimekuwa zikiwaunganisha zaidi
Watanzania kuiunga mkono CHADEMA bega kwa bega, ili kupata haki na
matumaini ya wanyonge, katika mapambano ya awamu ya pili, kuelekea uhuru wa kweli.

Imetolewa leo Novemba 30, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA*0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa