Na. Lilian Lundo –
MAELEZO
Mratibu Elimu Kata
(MEK) ni mmoja kati ya kiungo kikubwa kati ya ofisi ya elimu ya wilaya na shule
za Serikali katika ngazi ya kata ambaye ndiye mfuatiliaji mkubwa wa maendeleo
ya elimu ndani ya kata.
Shughuli nyingine
zinazofanywa na MEK ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya taalamu ya wanafunzi
katika kata yake, kukagua ufundishaji wa walimu, kufuatilia mahudhurio ya
wanafunzi pamoja na kusimamia vikao mbalimbali vya shule zilizoko katika kata
yake.
Asilimia kubwa ya
Waratibu Elimu Kata walikuwa wanashindwa kufikia malengo ya kazi zao kutokana
na changamoto ya usafiri, ambapo wengi wao walikuwa wakitumia usafiri wa
baiskeli ambao ha ukuwa usafiri
rafiki kutokana na kazi yao ya kukagua shule zote katika kata wanazozisimamia.
Serikali kwa kuliona
hilo, kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T)
ilitoa pikipiki kwa kila MEK katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi,
Shinyanga, Simiyu na Mara ili kurahisha ufuatiliaji wa mendeleo ya shule zao
kwa urahisi.
Pikipiki hizo
zimeleta mafanikio kwa kupunguza idadi ya wanafunzi watoro, kiwango cha ufaulu
kupanda kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara wa walimu pamoja na matatizo
kutatuliwa kwa haraka kufuatia taarifa za shule kufika ofisi za wilaya kwa
wakati.
Sweetbert Malimi ni
Mratibu Elimu Kata wa Sanzawa Wilaya ya Chemba, Mkoani Dodoma anasema kwamba
Pikipiki imemuwezesha kushughulikia kwa wakati matatizo yanayotokea katika
shule anazozisimamia tofauti na kipindi ambacho hakuwa na pikipiki.
Anaendelea kusema
kuwa, matatizo yalipokuwa yakitokea katika shule anazosimamia yalikuwa
yakimsubiri MEK hata kwa mwezi mzima. Lakini sasa hivi hali imekuwa tofauti
kutokana na urahisi wa kufikika kuzitembelea kutembelea shule zake hata mara
mbili kwa wiki.
Vilevile, Mratibu Malimi
amesema kuwa ameweza kukagua na kufuatilia kwa wakati maendeleo ya taaluma ya
wanafunzi pamoja na ufundishaji wa walimu ambapo kabla ya kuwa na pikipiki kulikuwa
na baadhi ya walimu walijisahau kutokana na kutokaguliwa mara kwa mara.
Anaendelea kwa kusema
kuwa, ufuatiliaji huo umeletea mafanikio makubwa katika Mkoa wa Dodoma, ambapo
ufaulu wa darasa la saba kwa wilaya ya Chemba peke yake ulipanda kutoka
asilimia 30 mwaka 2015 mpaka asilimia 46 mwaka 2016.
Kwa upande wake
Mratibu Elimu Kata wa Songambele iliyoko Wilaya ya Kongwa, Mkoani Dodoma
amesema kuwa katika kata yake ana shule Sita za kuzifuatilia ambapo kabla ya
kupata pikipiki alikuwa anatumia baiskeli kutembelea shule hizo na aliweza
kutembelea shule hizo mara moja kwa wiki.
Baada ya kupata
pikipiki anauwezo wa kutembelea shule hizo mara tatu hadi nne kwa wiki
akifuatilia maandalio ya walimu, maazimio ya kazi, utengenezaji wa zana za kujifunzia
na kufundishia, mahudhurio ya wanafunzi pamoja na kuhudhuria vikao vya kamati
ya shule.
Aidha, amesema kuwa
kutokana na ufuatiliaji huo wa mara kwa mara katika shule hizo kumepelekea
umakini mkubwa wa ufundishaji wa walimu kwa kufuata taratibu za ufundishaji
kama vile kuwa na maandalio, maazimio ya kazi pamoja na kuwa na zana za
ufundishaji.
Pia amesema kuwa kwa
kutumia pikipiki aliyopewa amekuwa akiwatembelea wazazi ambao watoto wao ni
watoro, na kuwashauri juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao na wazazi wenyewe.
Juhudi hizo zimepelekea wazazi wengi kubadilika na wamekuwa na mtazamo chanya
kwa kushirikiana na walimu katika kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya taaluma
ya watoto wao.
Nae, Mratibu Elimu
Kata wa Kagera Manispaa ya Kigoma Mkoani Kigoma
Jovitus Augustus anasisitiza kuwa kabla ya kupewa pikipiki kata yake
ilikuwa na changamoto ya utoro kwa wanafunzi pamoja na ufaulu duni wa wanafunzi
wa darasa la saba.
“Pikipiki niliyopewa
kupitia mpango wa EQUIP-T umeniwezesha kutengeneza mipango kazi ya wiki na
kuisambaza katika shule zote za kata pamoja na kufuatilia utekelezaji wake,”
alifafanua Jovitus.
Ameendelea kusema
kuwa pikipiki hiyo imemuwezesha kukagua utekelezaji na utoaji taaluma kwa
kukagua maazimio ya kazi na maandilio ya somo pamoja na kufanya vikao vya mara
mara kwa mara na walimu ili kupata maelezo ya walimu walioshindwa kutekeleza
wajibu wao.
Aidha, kupitia juhudi
hizo zilizofanyika, ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba shule za msingi za
kagera na Mgumile ulipanda pamoja na
mahudhurio ya walimu na wanafunzi katika kata hiyo umeongezeka.
Vilevile, umeanzishwa
utaratibu wa mitihani ya kata kwa darasa la saba pamoja na kuweka kambi kwa
wanafunzi wanaojiandaa na mitihani wa darasa la Saba.
Kwa upande wake
mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Mazoezi Bunda iliko Halmashauri ya Mji Bunda
Mkoa wa Mara, Mwalimu Vicent Ndunguru, aliipongeza Serikali kupitia Mpango wa
EQUIP-T kwa kutoa pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata ambao kwa kiasi kikubwa
umewarahisishia utendaji kazi wao.
Amesema kuwa mambo
mengi yalikuwa hayaendi yalivyotakiwa kuwa kutokana na MEK kutotembea shule
mara kwa mara kutokana na ukosefu wa usafiri wa uhakika.
Kupatiwa pikipiki MEK
imekuwa chachu ya kutembelea shule zilizochini ya kata yake mara kwa mara ili kufuatilia
maendeleo ya shule na kuwasilisha taarifa zake ofisi za elimu wilaya kwa wilaya
kwa wakati.
Mwalimu Ndunguru
ambaye pia ni Msaidizi wa MEK katika kata ya Nyasura amesema kuwa, MEK huyo
amekuwa msimamizi bora wa elimu kwa kuitisha vikao vya mara kwa mara kujadili
maendeleo ya shule katika kata yake, shule ya Msingi Mazoezi Bunda ndio eneo
lilochaguliwa kwa ajili ya kufanyia mikutano hiyo.
Ndunguru ameendelea
kusema kuwa, MEK huyo amekuwa chachu ya maendeleo ya shule zilizoko katika kata
hiyo hasa baada ya kuwa na uhakika na usafiri ambao kwa asilimia kubwa
umemuwezesha kufanya kazi zake kwa urahisi na hata kufikia malengo aliyowekewa
na mwajiri wake na yale aliyojiwekea yeye mwenyewe katika kuhakikisha ubora wa
elimu uaongezeka siku hadi siku kutoka ngazi ya kata mpaka Taifa.
Mwalimu Ndunguru ameishukuru
Serikali kwa jitihada ya kujali sekta ya elimu, na kuiomba Serikali kuendeleza
utaratibu wa ugawaji wa pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata wa mikoa mingine
iliyobaki ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi kama ambavyo wenzao waliopewa
pikipiki walivyoweza kufanikiwa kupandisha kiwango cha ufaulu na kukomesha
tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Serikali kupitia
mpango huo pia umetoa vishikwambi kwa Waratibu Elimu Kata hao, ambao wamekuwa
wakitumia vifaa hivyo kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa walimu wakuu wa
shule wanazozisimamia na wao kuzituma taarifa hizo ofisi za elimu za wilaya.
Mpango wa EQUIP-T tayari
umeshatoa jumla ya pikipiki 1,000 kwa Waratibu Elimu Kata wa mikoa ya Dodoma,
Kigoma, Lindi, Shinyanga, Simiyu, Shinyanga na Mara ambazo zilitolewa kati ya
mwaka 2014 na 2015 na wanawaezesha waratibu hao kupata fedha ya mafuta na
utengenezaji wa pikipiki hizo kila mwezi.
0 comments:
Post a Comment