Na Beatrice Lyimo – MAELEZO
07/09/2016
Serikali
imetoa wito kwa wanasiasa kutotumia masuala ya Muungano katika masuala
yao ya kiasisa kwani watu wa pande mbili za Muungano hawawezi kufarakana
kwa sababu ya umiliki wa eneo.
Akijibu
swali la Mhe. Jaku Hashim Ayoub lililohusu umiliki wa kisiwa cha Latham
(Fungu Mbarak), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) January Makamba amesema kuwa katika orodha ya changamoto 14
za Muungano zilizoshughulikiwa na zinazoendelea kushughulikiwa hakuna
suala lolote linalohusu umiliki wa eneo.
Waziri Makamba amesema hakuna mgogoro wowote unaohusu umiliki wa eneo lolote baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuwa tafsiri na suala zima la mipaka ya Jamhuriya Muungano
wa Tanzania na Zanzibar limewekwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano na Katiba ya Zanzibar.
Waziri
Makamba amesema kuwa kuhusu suala la mafuta na gesi hakuna mgogoro
wowote kwani leseni za utafutaji wa mafuta zilitolewa na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika eneo hilo kwa mujibu wa
Sheria ya Utafutaji Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 1980.
“Hakuna
mgogoro wowote wa mafuta na gesi baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huko nyuma
leseni za utafutaji mafuta zilitolewa na TPDC katika eneo hilo kwa mujibu wa Sheria ya utafutaji mafuta na gesi asilia,” amefafanua Waziri Makamba.
0 comments:
Post a Comment