SERIKALI imewataka wananchi na wadau katika Mikoa ya Lindi na Pwani kuendelea kulinda maeneo tengefu na hifadhi ya bioanuai ili yaendelee kubaki na ubora na viwango vilivyoainishwa kitaifa na kimataifa.
Hayo
yamesemwa Julai 19, 2024 Wilayani Rufiji Mkoani Pwani na Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
wakati alipokuwa akizindua hifadhi hai ya Rufiji- Mafia- Kibiti-Kilwa
(RUMAKI).
Mhe. Khamis amesema mifumo ikolojia iliyopo katika Hifadhi Hai ni miongoni mwa bioanuai muhimu za Ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki inayohifadhi bioanuai nyingi na za kipekee zinazotambulika kitaifa na kimataifa.
”Tunapaswa
kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Hifadhi Hai hii inabaki
kuwa kwenye ubora na viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa vigezo vyetu
vya ndani na vya UNESCO” amesema Khamis.
Ameongeza kuwa Hifadhi
Hai ya RUMAKI ni kielelezo kizuri cha juhudi nyingi zilizofanywa na
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mashirika ya
kimataifa kwa miaka mingi ambayo inaenda sambamba na dhamira na malengo
ya uhifadhi maeneo tengefu, hifadhi ya malikale na bioanuai.
Aidha
Mhe. Khamis amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali Kutayarisha
mipango endelevu na shirikishi ya kulinda, kuhifadhi na kuendeleza
hifadhi hiyo ili iendelee kubaki katika ubora wake.
Naibu
Waziri Khamis amehimiza wananchi kujiepusha na uharibifu wa mazingira
ikiwemouchomaji moto, ukataji misitu ikiwemo mikoko na uvuvi haramu na
kuitaka NEMC kutumia mfumo maalum wa tahadhari za majanga ndani ya
hifadhi hizo.
Amefafanua kuwa iwapo hifadhi hai ya RUMAKI itaendelea
kulindwa na kuhifadhiwa kwa kuzingatia viwango na vigezo vya kitaifa na
kimatifa itasaidia shughuli endelevu za kijamii, kiuchumi, kitalii na
kimazingira na hivyo kubaki katika mtandao wa Hifadhi Hai Duniani.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Menan Jangu amewapongeza
wananchi wa Wilaya za Rufiji, Mafia na Kilwa kwa kuendelea kutunza
mazingira juhudi ambazo zimeweza maeneo hayo kutambulika kimataifa.
Amesema
NEMC itaendelea kuratibu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira
kupitia kwa wananchi na taasisi mbalimbali na kuanisha maeneo yote yenye
sifa na vigezo vya kutambulika kimataifa.
”Tunapokuwa
na eneo la hifadhi hai lina sifa na malengo makuu matatu ambayo ni
maendeleo endelevu, uhifadhi na utunzaji wa viumbe hai vinavyotunzwa kwa
faida ya vizazi vya sasa na baadae” amesema Dkt. Menan.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira ulimwenguni (WWF),
Bi. Joan Itanisa amesema ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga
mkono juhudi za Shirika hilo katika uendelezaji wa miradi ya uhifadhi na
usimamizi wa mazingira nchini.
Ameongeza
kuwa uzinduzi wa hifadhi hiyo ni moja ya ahadi zilizowekwa na Wakuu wa
Nchi mbalimbali duniani kuwa ifikapo mwaka 2030 asilimia 30 ya eneo la
dunia iwe imehifadhiwa na kupongeza juhudi utayari wa Tanzania katika
kutekeleza azimio hilo.
“Uzinduzi
wa RUMAKI ni ishara kuwa Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuwa
kinara wa masuala ya uhifadhi...Tutaendelea kushirikiana na Serikali
katika kuhakikisha wananchi wanaozunguza hifadhi hizi wanapata manufaa
kutokana na uhifadhi huu” amesema Itanisa.