Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
2/2/2015 Wakazi wa mkoa
wa Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu
la wapiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni
mwa mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa jana
na Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jerry Silaa
wakati akiongea kwenye kilele cha sherehe za kutimiza miaka 38 ya chama
hicho mkoani Lindi zilizofanyika katika tawi
la Mnazi Mmoja lililopo kata ya Mingoyo
wilaya ya Lindi mjini.
Silaa mbaye pia ni Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala alisema iwapo mtu atajiandikisha katika daftari la kudumu la
wapiga kura atashiriki katika uchaguzi mkuu ujao hivyo basi wakati
ukifika ni jukumu la mabalozi kuwahimiza
wananchi
kujiandikisha ili wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Aidha Meya Silaa aliwapongeza wana CCM kwa ushindi wa asilimia 77 walioupata
wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana na
kuwataka kuwa makini katika kuteua viongozi wanaokubalika na wananchi na kuachana na makundi yanayokibomoa chama
hicho kwa kufanya hivyo itawawezesha kupata ushindi
wa kishindo katika uchaguzi ujao.
Kwa upande wa vijana aliwahimiza
kujishughulisha katika shughuli za kimaendeleo ili waweze kujipatia maendeleo kwani mkoa
wa Lindi uko katika dira ya maendeleo kwa kuwa na ardhi yenye rutuba, barabara nzuri na gesi.
Silaa alisisitiza, “Nawashauri
vijana wenzangu mjiunge na CCM chama kinachowasaidia vijana kuwaletea
maendeleo ukilinganisha na vyama vingine vinavyowapotezea muda na kurudisha
nyuma maendeleo yenu”.
Alikipatia kikundi cha ujarisiamali
cha Zamira ambacho kinajishughulisha na shughuli za kilimo cha mikorosho,
mihogo, karanga na kunde shilingi laki tano ili ziweze kuwasaidia kununua
pembejeo za kilimo.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete alisema sherehe hizo zina umuhimu
wa kipekee kwa wana CCM kwani zimeangukia mwaka wenye matukio muhimu na makubwa
kwa nchi ambayo ni kura ya maoni ya
katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema
mwaka 2015 ni mwaka wa kuhitimisha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka
2010-2015 ambapo Chama hicho kiliwaomba wananchi wakichague ili kiwafanyie kazi
watanzania ambao walikiamini na kukichagua.
“Matokeo yake
watanzania wameyaona , miundombinu ya barabara, shule na vyuo vimejengwa na watoto wengi hivi sasa wapo mashuleni.
Huduma za afya zimeboreka kwa kujengwa Hospitali, vituo vya afya na Zahanati”.
Lakini hata kwa yale
ambayo hayakuwepo kwenye Ilani na yalikuwa ni matakwa ya wananchi chama chetu
sikivu hakikusita kuyakubali kwani yalikuwa ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa na
vizazi vyetu”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu Katiba
inayopendekezwa MNEC huyo alisema itapigiwa kura ya maoni mwaka huu mwezi wa nne
hivyo basi aliwataka wanaCCM na watanzania wote kwa ujumla kuipigia kura ya
ndiyo katiba pendekezwa kwani inakidhi matakwa ya watanzania kwa kuwa imegusa
katika maeneo yote.
Akiwasalimia wananchi
waliohudhuria sherehe hizo Mkuu wa wilaya ya Lindi Dkt. Nassoro Hamidi aliwahimiza
wazazi kuhakikisha watoto walioandikishwa darasa la kwanza na wale waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza wanaenda shule kuanza masomo ili waweze kupata
elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Katika kilele cha
sherehe hizo zilizoenda sambamba na wiki ya Chama na Jumuia zake kauli mbiu
yake ni Umoja ni ushindi, Katiba yetu, Taifa letu jumla ya wanachama wapya 448 walijiunga na
chama hicho ambapo saba walitoka vyama vya upinzani, Chama cha Wananchi (CUF) watano na Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wawili.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment