Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu
wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi akizungumza na ugeni kutoka Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wakati walipomtembelea ofisini kwake
mjini Lindi.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akitambulisha
msafara wake kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi (hayupo
pichani) wakati walipomtembelea ofisini kwake mjini Lindi. Kushoto ni
Meneja Mikopo, Bw. Samuel Mshote na Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa
TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha (katikati).
Mkurugenzi
wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha
(aliyesimama) akiwasilisha mada juu ya fursa za mikopo zinazotolewa na
Benki ya Kilimo kwa Wadau wa Korosho na Ufuta Mkoa wa Lindi uliofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Wadau wa Korosho na Ufuta Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Mkuu
wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi ameiomba Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) kukopesha wakulima wa mazao ya ufuta na mihogo
ili waweze kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara hasa kwa wakulima
wadogo wadogo wa mkoani humo.
Bw.
Zambi alitoa wito huo wakati wa mkutano wa Wadau wa Korosho na Ufuta
Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Lindi.
Bw.
Zambi alisema kuwa mkoa wa Lindi ni mkoa uliojaaliwa katika kuzalisha
mazao ya ufuta na mihogo lakini changamoto kubwa ni mtaji wa kulima
kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
“Wakulima
wa mkoa wa Lindi wapo tayari kushiriki katika kuleta mapinduzi ya
Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara lakini kwa sasa
suala la mtaji wa kilimo cha kibiashara ni changamoto kubwa,” alisema
Bw. Zambi.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
alisema kuwa Benki ya kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa wakulima wadogo
wadogo waliokuwa kwenye vikundi ili waweze kukopeshwa.
Bw.
Assenga aliongeza kuwa Benki ya Kilimo pia ipo tayari kuwekeza kwenye
miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa kuipatia mikopo yenye riba nafuu
zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko.
“Kwa
kutambua umuhimu wa wakulima wadogo wadogo nchini TADB imedhamiria na
kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta
Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia
upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia
maendeleo ya kilimo nchini,” alisema.
Naye,
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema
kuwa TADB inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma zisizo za kifedha kwa
wakulima kama vile kujengewa uwezo juu ya uandaaji wa andiko la miradi
ya Kilimo, pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko, usimamizi wa
biashara, mafunzo juu ya miradi ya Kilimo na mbinu za majadiliano ya
mikataba.
“Tupo
tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa
na Serikali kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji,
miundo mbinu ya umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo,” alisema.
Bw.
Chacha aliongeza kuwa kwa upande wa mikoa ya kusini Benki ya Kilimo
imejipanga kueendeleza miundombinu ya umwagiliaji na maghala pamoja na
uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo na kuimarisha
viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta, mihogo.
Bw.
Chacha aliongeza kuwa Benki imejipanga kuwezesha uanzishaji wa mashamba
mapya na ya kisasa ya mihogo, korosho na ufuta mkoani Lindi.
Chanzo Michuzi Blog
0 comments:
Post a Comment